Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Dkt. Mpango Aagiza Ujenzi wa Kituo cha Kupoozea Umeme wa Gridi ya Taifa cha Inyonga Kukamilika Oktoba, 2023
Jul 21, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa. Dkt. Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Nishati kuhakikisha ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme wa Gridi ya Taifa cha Inyonga kukamilika ifikapo Oktoba mwaka 2023 na Mkoa wa Katavi unaunganishwa katika Gridi ya Taifa.

Makamu wa Rais amesema hayo alipokuwa akizungumza na viongozi na wananchi wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa  msongo wa Kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi katika eneo la Inyonga Wilaya ya Mlele. Makamu wa Rais ameonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo ambao umechelewa kwa takribani miezi nane mpaka sasa.

Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka Wakurugenzi kuacha mara moja tabia ya kutoza ushuru kwa mazao yanayosafirishwa chini ya tani moja kwani Serikali iliondoa tozo hizo ili kuwasaidia wakulima wadogo kupata kipato. Amesema Wakurugenzi wanapaswa kutafuta mbinu sahihi za kuwabaini wanaokusanya mazao zaidi ya tani moja ili kuwanusuru wale wakulima wadogo.

Pia, Makamu wa Rais amewaasa wananchi wa Mlele kuendelea kutafuta elimu kuhusu lishe ili wananchi wa mkoa huo wawe na afya bora kulingana na mazao mengi wanayozalisha. Makamu wa Rais amewataka kuendelea na juhudi za kutunza mazingira ikiwemo kupiga vita uchomaji miti na uchafuzi wa mazingira.

Makamu wa Rais amewaagiza wazazi na walezi Mkoa wa Katavi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ili taifa kuwa na rasilimali bora zaidi itakayoharakisha maendeleo.

Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mheshimiwa Mwamvua Mrindoko ameishukuru Serikali kwa kuuwezesha mkoa huo kwa miradi mbalimbali inayochochea maendeleo kama vile miradi ya elimu, maji, barabara, afya pamoja kuongezewa idadi ya watumishi wapatao 692 katika sekta ya afya na elimu kwa mara moja.

Awali akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Mlele, Mbunge wa Jimbo hilo, Mheshimiwa Isaac Kamwele ameiomba Serikali kukamilisha ujenzi wa majosho sita ili kuwasaidia wananchi wa eneo hilo ambao wengi wao ni wakulima na wafugaji. Pia ameongeza kwamba kutokana na kuongezeka kwa idadi ya wananchi wananchi hao wanahitaji shule mbili zaidi za elimu ya msingi pamoja na Chuo cha Veta kitakachowasaidia katika kupata ujuzi.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yupo ziarani mkoani Katavi ambapo anakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi