Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Dkt. Mabula Awataka Waandishi Kuwa Jicho la Serikali Kutoa Elimu ya Sekta ya Ardhi
May 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amewataka Waandishi wa Habari nchini kutumia nafasi zao vizuri kuwa kama jicho la Serikali katika kutoa elimu na ufahamu kwa wananchi kuhusu sekta ya ardhi.

Aidha, amewataka kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inapungua kwa asilimia 100 kama siyo kutokuwepo kabisa katika jamii. 

Kauli ya Waziri wa Ardhi inakuja huku kukiwa na taarifa za upotoshaji zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii hasa mtandao wa Jamii Forum kueleza kuwa migogoro ya ardhi imeanza kushamiri upya. 

Dkt Mabula alisema hayo Mei 23, 2022 wakati wa mkutano wa majadiliano ya kisekta kati ya wadau Wizara na wadau wa sekta ya ardhi uliofanyika jijini Dar es Salaam.

 ‘’Ofisi zipo wazi pale mtakapotaka ufafanuzi wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya ardhi tushirikiane katika kutoa elimu ili kutokomeza migogoro ya ardhi’’, alisema Dkt. Mabula

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, Wizara yake iko tayari muda wowote kupokea na kuchakata mapendekezo yanayoweza kuendelea kuleta mapinduzi katika sekta ya ardhi nchini. 

Wizara ya Ardhi ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za utatuzi wa changamoto za sekta ya ardhi ikiwemo kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma za ardhi, kuendelea kuimarisha na kuziwezesha ofisi za ardhi za mikoa katika kuhakikisha huduma zinapatikana karibu na wananchi.

Aidha, katika juhudi za kurahisisha utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa wananchi, Wizara ya Ardhi imeanzisha Kituo cha Mwasiliano kwa Wateja ambapo wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao kwa njia ya simu na kutafutiwa ufumbuzi bila kufika ofisi za ardhi.

‘’Sekta ya ardhi ni moja ya nguzo muhimu ya kuwezesha kuleta maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla na utekelezaji wa majukumu ya sekta hiyo utawezesha shughuli mbalimbali za sekta nyingine na kukuza uchumi wa kipato cha kati kupitia uwekezaji katika ardhi’’. Alisema Dkt Mabula.

Alieleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kufanya maboresho kwenye sekta ya ardhi kwa kutunga na kusimamia sera na sheria mbalimbali sambamba kuandaa kanuni, miongozo na kuratibu utekelezaji wa mikakati mbalimbali ndani ya sekta kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa milki salama za ardhi kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii.

Pia Waziri wa Ardhi alisema sekta ya ardhi imeendelea kuwa kiungo wezeshi kwa sekta nyingine za uzalishaji zikiwemo viwanda, kilimo, mifugo miundombinu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi