Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Dkt. Mabula Ataka Uwajibikaji kwa Makamishna wa Ardhi Kufikia Malengo ya Wizara
Feb 25, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM ARUSHA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amewataka Makamishna Wasaidizi wa Ardhi wa mikoa nchini kuwajibika na kutumia wajibu wao katika kutekeleza mikakati ya Wizara kufikia malengo.

Aidha, amewataka Makamishna hao kuwapangia majukumu kwa malengo maafisa walio chini yao na kufuatilia kazi wanazowapa mara kwa mara.

Dkt. Mabula amesema, hayo tarehe 25 Februari 2022 wakati akifungua kikao kazi cha Menejimenti na Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa kilichofanyika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.

“Yapo malalamiko ya lugha zisizofaa kwa wateja hii haikubaliki, fuatilieni hili na kulikemea vikali na kuzingatia misingi na kanuni za Utumishi wa Umma katika majukumu yenu ya kila siku”, alisema Dkt. Mabula.

Aidha, aliwataka katika utekelezaji mpango mkakati wa wizara wanazingatia vipaumbele vya serikali hususan maelekezo ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan na ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

Akigeukia suala la makusanyo ya kodi ya pango la ardhi, Waziri wa Ardhi aliwataka Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa kuwa wabunifu katika njia za kukusanya mapato.

“Suala la mtandao kutopatikana muda mwingi linaonekana kuwa kikwazo katika ukusanyaji maduhuli, lifanyieni kazi” alisema Dkt. Mabula.

Waziri Dkt. Mabula pia alihimiza kuongezwa kwa kasi ya umilikishaji ardhi kwa wananchi na kuwataka Makamishna hao na Wakuu wa Idara kuweka malengo kwa kila ofisa mwenye taaluma ya ardhi kuandaa hati.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Allan Kijazi alisema, baada ya kuteuliwa katika nafasi ya Katibu Mkuu alifanya ziara kwa baadhi ya mikoa na kubaini changamoto kadhaa alizozitaja kuwa ni pamoja na kutofikiwa kwa malengo ya ukusanyaji kodi ya ardhi pamoja na baadhi ya halmashauri kutohudumia idara za ardhi kwa madai ya idara hizo kuhamishiwa wizarani.

“Nimeanza kuchukua hatua ili kutatua changamoto hizo ambapo tayari nimetoa maagizo mbalimbali kwenye Mikoa na Menejimenti ya Wizara na ni matarajio yangu kikao kazi hiki kitaibua suluhisho la changamoto hizo”, alisema Dkt. Allan Kijazi.

Kwa mujibu wa Dkt. Kijazi, Wizara ya Ardhi imekuwa ikinyooshewa vidole na wananchi kwa masuala ya ukiukwaji wa haki za wananchi na kuchafua taswira ya Wizara na kutaka watendaji wa sekta hiyo kujitafakari na kujisahihisha kwa kutimiza wajibu ili kuondoa dhana hiyo.

Aligusia pia mpango wa urasimishaji makazi holela na kueleza kuwa, ni matarajio yake kupitia kikao hicho, washirikia wake wataibuka na mkakati wa uelekeo wa wizara katika kupanga miji sambamba na usimamizi wa fedha kiasi cha shilingi Bilioni 50 zilizotolewa kwa ajili ya mpango wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi maarufu kama KKK.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi