Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watanzania Waalikwa Ibada ya Kumbukizi ya Hayati Sokoine
Mar 28, 2024
Watanzania Waalikwa Ibada ya Kumbukizi ya Hayati Sokoine
Msemaji wa Familia ya Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Lembris Kipuyo akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma kuhusu kufanyika kwa ibada ya kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Sokoine itakayofanyika Aprili 12, 2024 katika Kijiji cha Enguik, Monduli Juu mkoani Arusha ambapo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan atawaongoza viongozi wa serikali na watanzania katika tukio hilo.
Na Lilian Lundo – Maelezo

Familia ya Hayati Edward Moringe Sokoine aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewaalika Watanzania katika ibada ya kumbukizi ya miaka 40 ya kiongozi huyo, itakayofanyika Aprili 12, 2024 katika Kijiji cha Enguik, Wilaya ya Monduli, mkoani Arusha.

Msemaji wa familia ya Hayati Edward Moringe Sokoine, Bw. Lembris Marangushi Kipuyo amesema hayo leo Machi 28, 2024 jijini Dodoma, wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu kumbukizi ya miaka 40 ya kiongoozi huyo.

“Nawaalika Watanzania wote kwenye ibada maalum ya kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itakayofanyika Aprili 12, 2024, katika Kijiji cha Enguik, Monduli Juu mkoani Arusha. Ibada hiyo itakafanyika siku ya Ijumaa Aprili 12, 2024, saa 3:00 asubuhi, imeandaliwa na familia ikishirikiana na Taasisi ya Hayati Edward Moringe Sokoine,” amesema Bw. Kipuyo.

Waandishi wa Habari wa  jijini Dodoma waliohudhuria mkutano uliohusu kumbukizi ya miaka 40 ya Hayati Sokoine itakayofanyika Aprili 12, 2024 katika Kijiji cha Enguik, Monduli Juu mkoani Arusha ambapo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan atawaongoza viongozi wa serikali na watanzania katika tukio hilo.

Amesema ibada hiyo ya kumbukumbu ya Hayati Sokoine itawashirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali wakiongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Aidha, amesema kuwa, Hayati Sokoine alikuwa mzalendo wa kweli, alipenda taifa lake na wananchi wake, alihakikisha kwamba rasilimali za nchi zinatumika na Watanzania wote, aliwatumikia wananchi bila kubagua na alikuwa na hofu ya Mungu katika kufanya kazi zake.

Hayati Sokoine alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vipindi viwili wakati wa uongozi wa Awamu ya Kwanza. Alizaliwa Agosti 01, 1934, kijijini Enguik, Monduli Juu wilayani Monduli, mkoani Arusha.


 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi