Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wataalamu Watakiwa Kutekeleza Sera ya Mazingira
Oct 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Serikali imewataka wataalamu kutoka wizara za kisekta kutekeleza Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021 ili kuwa na usimamizi thabiti wa matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua Warsha ya kukuza uelewa kwa wataalam hao kuhusu usimamizi wa matumizi salama ya Bioteknolojia ya kisasa leo Oktoba 27, 2022 jijini Dodoma.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga, Dkt. Mkama alisema ni muhimu kujenga uwezo wa taasisi na kukuza uelewa wa jamii kuhusu teknolojia hii ili kuhakikisha tunafaidika na teknolojia hii katika sekta husika na kupunguza uwezekano wa kutokea kwa athari zozote za afya ya binadamu na mazingira.

Alisema wataalamu hao wana jukumu la kutoa ushauri stahiki kuhusu masuala haya ili Serikali kwa kuzingatia vipaumbele na maslahi ya nchi inapofikia maamuzi ya matumizi ya teknolojia hii katika sekta yoyote nchini.

“Katika kuhakikisha kunakuwa na usalama wa matumizi ya bioteknolojia ya kisasa nchini, Serikali imeandaa na kuweka nyenzo mbalimbali za usimamizi wa teknolojia hii ikiwa ni pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Mfumo wa Kitaifa wa Usimamizi wa Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa 2007, Kanuni za Matumizi Salama ya Bioteknolojia ya Kisasa ya mwaka 2009 na marekebisho yake ya mwaka 2015 na Miongozo mbalimbali za mwaka 2010,” alisema.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu huyo amebainisha kuwa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Kimataifa ya Hifadhi ya Bioanuai ambao una malengo makuu matatu yakiwemo Hifadhi ya bioanuai, Matumizi endelevu ya bioanuai na Mgawanyo sahihi wa faida zitokanazo na matumizi ya bioanuai.

Aliongeza kuwa Tanzania iliridhia Mkataba huu Machi 1996 ili kuweza kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika kutekeleza malengo hayo.

Pia, alisema Ibara ya 19 ya Mkataba huu, inaainisha, umuhimu wa nchi wanachama kuweka mazingira wezeshi ya kutumia bioteknolojia ya kisasa kwa maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Prof. Peter Msolla, Mwenyekiti wa Chama cha Bioteknolojia nchini alisema warsha hiyo ni muhimu kwani inakutanisha wataalamu mbalimbali kuweza kubadilishana mawazo ili mwisho wa siku kupata maamuzi yenye tija.

Alisema bioteknolojia sio mpya ni tasnia ya zamani ambayo imekuwa ikibadilika kadri ya wakati na haina tofauti sana na uzalishaji wa mazao kwa njia ya kiasili lakini tofauti yake kubwa ni muda wa matokeo.

Nae Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba alisema tunahitaji mijadala mingi zaidi kuhusu usimamizi wa matumizi salama ya bioteknolojia ya kisasa ili kuweza kufanya maamuzi sahihi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi