Na Tiganya Vincent-Urambo, Tabora
Walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini wametakiwa kuhakikisha wanatimiza masharti ya elimu na afya ili kuepuka kukatwa fedha ambazo wanastahili kupata kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa ajili ya kuwahuduma watoto wao.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Afisa Uhawilishaji Fedha kwa njia ya Mtandao wa TASAF, Bibi Kweji Kasulende wakati akijibu malalamiko kutoka kwa wakazi wa maeneo mbalimbali Wilayani Urambo, ambao wamekatwa fedha zao kwa sababu ya kukosekana taarifa zinazoonesha kuwa waliwapeleka watoto wao kliniki na wengine wanahudhuria shule bila kukosa.
Bibi Kasulende aliongeza wengine wamekuwa wakikatwa fedha kwa sababu ya watoto wao kutohudhuria shule au wakati mwingine majina waliwaandikisha shuleni kuwa tofauti na yale yalipo katika mpango wa TASAF.
Alisisitiza umuhimu wa walengwa kuhakikisha taarifa zilizopo TASAF zinawiana na zile za shule na vile vile kuhakikisha kuwa wanapowapeleka watoto wao kliniki taarifa ya mahudhurio zinaonekana katika kumbukumbu za Mfuko huo ili kuwaondolea usumbufu usio wa lazima.
“Ili kuondoa malalamiko hayo ni vema walezi au wazazi wa watoto mkahakikisha mnawapeka kliniki watoto wenu walio chini ya miaka mitano na wale wanaosoma waende shule bila kukosa na kufuatilia mahudhurio yao siku zote za masomo” alisisitiza Kasulunde.
Bibi Kasulende alisema hatua hiyo itasaidia kuaondoa usumbufu ambao wamekuwa wakiupata kutokana na kukatwa fedha kwa sababu ya wao kushindwa kabisa kurekebisha taarifa zao zinahusua masuala ya elimu na mahudhurio ya kliniki ya watoto wao.
Kwa upande wa Mratibu wa TASAF Mkoani Tabora Bw. Ngoko Buka aliwatoa hofu walengwa wote wa mpango huo ambao wamekatwa fedha zao kwa sababu ya kushindwa kurekebisha taarifa za watoto na kuwaeliza kuwa wakishazifanyia marekebisho fedha yao zitalipwa katika awamu ijayo.
Aliwataka kutumia wajumbe wa Kamati za Jamii za Utekelezaji wa Mpango(CMC) kuhakikisha wanawasaidia Walengwa kurekebisha kasoro zilizopelekea wao kukatwa fedha ambazo kimsingi walipaswa walipwe.
Bw. Buka aliwaomba walengwa kuhakikisha kila mtoto anapotoka hatua moja kwenda nyingine wanapeleka taarifa katika Ofisi husika ili kuepuka makosa ya aina hiyo kujirudia tena na kujikuta wakipata pesa pungufu.
Katika hatua nyingine baadhi ya walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikimi wameishukuru TASAF kwa kuwawezesha kifedha jambo lililowasaidia kusomesha watoto wao na kuwahudumia katika masula ya sare na kodi za Hosteli.
Mmoja wa Walengwa hao Bibi Yasinta Emmanuel alisema kuwa fedha hizo zimemsaidia katika kusomesha watoto wake wawili Shule ya Msingi na kuanzisha mradi mdogo wa ufugaji wa kuku na ununuzi wa mabati sita kwa ajili kuezekea nyumba yake.
Mlengwa mwingine Mohamed Juma alisema kuwa fedha alizozipokea kutoka TASAF chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini zimemsaidia kuanzisha mradi wa ufugaji wa nyuki kwa ajili ya uzalishaji wa asali.
Alisema kuwa hadi hivi sasa anayo mizinga 19ambapo kati ya hiyo 9 ni ya kisasa na iliyobaki ni ile ya kienyeji.