Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanaoishi Maeneo Hatarishi Chemba Kuhamishwa
Jan 18, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na; Mwandishi Maalum.

SERIKALI wilayani Chemba mkoani Dodoma imesema kuwa imepanga kuwahamisha watu wanaoishi maeneo hatarishi ya kupata mafuriko kutokana na zaidi ya Kaya 2,000 kuzungukwa na maji katika kata ya Mrijo hadi hivi sasa.

Akiongea wakati akitoa taarifa kwa Waratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu waliokwenda kufanya tathmini ya maafa yaliyotokana na mafuriko ya mvua zinazoendelea kunyesha wilayani humo, Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga alibainisha kuwa mkakati wa muda mrefu walionao ni kuwatafutia wakazi hao maeneo salama.

Odunga alisema kuwa kwa sasa Kamati za Maafa zimechukua hatua ya kukabili maafa ya mafuriko kutokana na  idadi ya nyumba zilizozungukwa na maji kuongezeka siku hadi siku kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha hivyo wameanzisha kambi maalum kwa watu ambao nyumba zao zimeanguka kutokana na maafa hayo.

Aliongeza kuwa msaada wa haraka unahitajika kutokana na waathirika hao wa mafuriko kutumia  baadhi ya majengo ya madarasa ambayo yanapaswa kutumiwa na wanafunzi ambao wanajiunga na masomo mwaka huu.

“kwa sasa tunahitaji sana mahema, mataulo, mashuka , chakula pamoja na madawa kwajili ya kuwahudumia hawa watu ambao tunao hapa na tukipata vifaa hivyo basi tutaondoka hapa na kwenda kutengeza kambi sehemu nyingine ambayo tumeiandaa maaluum kwajili ya kuwahifadhi hawa watu na kuacha haya madarasa kwajili ya matumizi ya wanafunzi” alisema Odunga.

Odunga aliongeza kuwa tayari wilaya imeshaunda kamati mbalimbali ambazo zinahusika katika kusaidia wahanga hao kuwa salama kiafya kwa kuchukua tahadhari zinazoweza kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.

Naye Mratibu wa Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Ally Mwatima, alisema kuwa mahitaji yote ambayo yameanishwa na mkuu huyo wa wilaya wameyachukua na watayawasilisha ili hatua ziweze kuchukuliwa mapema iwezekanavyo.

“Kwanza niwapongeze kwa kukabili maafa kwa mujibuwa sheria,kanuni namiongozo ya menejimentiya maafa, hali hii  imesaidia kuokoa maisha ya hawa wenzetu na mahitaji yote mliyobainisha ni ya msingi sana hivyo tutakwenda kuonana pia na kamati ya maafa mkoa ili kuweza kuona na sisi tunaongeza nguvu katika vitu gani vya msingi ambavyo vitawasadia hawa wenzetu”alisema Mwatima.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi