Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waliopewa Maeneo Kulima Miwa Watakiwa Kuanza Kuyalima
Aug 22, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_9864" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage (kushoto) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati akielezea kuhusu mikakati wa Serikali ya Tanzania ya viwanda na mpango kazi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) mapema hii leo jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kikanda wa SADC, Bi. Sekela Mwaisela. (Picha na Eliphace Marwa).[/caption]

Na Jacquiline Mrisho.

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewataka wawekezaji waliopewa ardhi kwa ajili ya kilimo cha miwa waanze mara moja kulima zao hilo ili kupata malighafi kwa ajili ya uzalishaji wa sukari.

Waziri Mwijage ametoa wito huo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Mkakati wa Viwanda na Mpango Kazi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Amesema kuwa nchi wanachama wa SADC wanaruhusiwa kuingiza bidhaa bure nchini Tanzania na moja ya bidhaa hizo ni sukari ambayo kwa namna moja au nyingine sukari hiyo ikiruhusiwa kuingia itaua viwanda vichanga vilivyopo nchini.

“Ili kuweza kuviendeleza viwanda vyetu vya sukari ni lazima waliopewa maeneo ya kulima miwa wayatumie kikamilifu ili viwanda vyetu vizalishe sukari kwa wingi hali itakayotufanya tuache kabisa kutegemea sukari kutoka nje ya nchi. Kama kuna mkulima yeyote wa miwa aliyekwama kwa namna yoyote ile afike wizarani kwangu ili tujue namna ya kumsaidia,” amesisitiza Waziri Mwijage.

Waziri Mwijage ameongeza kuwa Tanzania ina fursa ya kuzalisha sukari tani milioni mbili kwa mwaka lakini hadi sasa inazalisha tani 302,000 hivyo kama Watanzania watatumia vizuri mabonde yaliyopo nchini wataweza kufikisha tani hizo zinazotakiwa.

Amefafanua kuwa mkakati wa SADC hautofautiani na mpango wa miaka mitano wa Tanzania unaoelekeza kuwekeza zaidi katika kulima chakula na kukiongeza thamani hivyo SADC inahimiza nchi zilizopo kwenye jumuiya hiyo kuzalisha kwa wingi na kuuziana wenyewe kwa wenyewe ndani ya Jumuiya.

Aidha, katika kutekeleza Mkakati wa Viwanda, Tanzania kupitia Sekretarieti ya SADC imepata ufadhili wa kiasi cha Euro milioni 1.4 kutoka mfuko wa Jumuiya ya Ulaya  utakaosaidia kuendeleza  miradi  minne ukiwemo mradi wa kupitia upya Sera ya Viwanda na kuwezesha mnyororo wa thamani wa zao la alizeti.

Katika Mkutano wa 37 wa Nchi Wanachama wa Jumuiya Maendeleo Kusini Afrika uliomalizika hivi karibuni nchini Afrika Kusini ambapo moja ya mambo yaliyosisitizwa ni kuzalisha bidhaa kwa wingi na kutengeneza soko kubwa ndani ya Jumuiya hiyo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi