Wakuu wa Mikoa na Wakuu Wilaya zote nchini wamesisitizwa kusikiliza kero za wananchi ikiwa ni hatua ya kurejesha uwajibikaji wa kidemokrasia nchini ulioasisiwa na serikali wa awamu iliyopita.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo jijini Dar es Salaam alipowaapisha wasaidizi wake aliowateua hivi karibuni baada ya kuwatengua wengine ambao walionekana wakiwapuuza wananchi wanaotumia uhuru wa kujieleza kueleza kero zao ili zipatiwe ufumbuzi.
“Makonda amezunguka mmeona mfano, wananchi wana kero kadhaa, nyingine nyepesi tu za kutatuliwa. Kule chini hawasikilizwi na wasiposikilizwa zile ndizo kura zetu, msipowasikiliza akipita mwingine akawaambia mimi nitawasikiliza watampa kwamba sisi tumewapuuza hatuwasikilizi. Niwasisitize sana [wakuu wa mikoa na wilaya] kusikiliza wananchi," ameelekeza Mkuu wa Nchi.
Pamoja na hilo, Rais Samia amearifu kwamba serikali anayoiongoza ina madeni mengi, hivyo anajipanga kupunguza ukopaji huku akiongeza ukusanyaji wa mapato ili miradi ya maendeleo itekelezwe kwa fedha za Watanzania wenyewe kama ilivyokuwa awamu iliyopita.
“Tunakwenda kupunguza masuala ya kukopa hasa kwa huduma za jamii kwa sababu katika miaka mitatu hii, tumekopa sana kwa ajili ya huduma za jamii; elimu, afya, umeme, maji na mambo mengine. Sasa tunakwenda miaka miwili hii, mwaka huu na mwakani, mnajua fika matumizi yataelekea wapi. Sasa ili fedha ziweze kurudi TAMISEMI lazima tufanye jitihada za kukusanya mapato," amefahamisha Mkuu wa Nchi.
Tangu alipoingia madarakani Machi 19, 2021 Rais Samia amekuwa akihakikisha miradi ya maendeleo aliyoiacha mtangulizi wake inaendelea kwa ufanisi mkubwa huku akitengua teuzi za wateule wazembe na wanaokosa uadilifu.