Jumla ya wagonjwa 361,894 huku watu wazima wakiwa 331,557 na watoto 30,337 wametibiwa kwa kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Sita katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam.
Kati ya wagonjwa hao 361,894 waliotibiwa katika taasisi hiyo, wagonjwa waliolazwa walikuwa 13,325 huku watu wazima wakiwa 10,781 na watoto 2,544.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge wakati akiongea na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika taasisi hiyo kwa kipidi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Kisenge alisema taasisi hiyo iliwatibu wagonjwa 316 kutoka nchi za Somalia, Malawi, Kenya, Rwanda, Visiwa vya Comoro, Msumbiji, Nigeria, Siera Leone, Zimbabwe, Zambia, Uganda, Congo, Ethiopia, Burundi na wengine kutoka nje ya Afrika zikiwemo nchi za Armenia, China, Ujerumani, India, Norway, Ufaransa na Uingereza.
Alisema wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua na kubadilishwa valvu za moyo moja hadi tatu, upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery –CABG), upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu walikuwa 2,161 kati ya hao watu wazima walikuwa 1,257 na watoto 904.
“Upasuaji mpya wa moyo wa kufungua kifua uliofanyika ni wa kurekebisha mshipa mkubwa wa damu uliotanuka kwenye kifua na tumbo, kurekebisha mshipa uliotanuka kwenye bega, kupandikiza mishipa ya damu wakati moyo unafanya kazi bila ya kuusimamisha moyo”.
“Kukarabati mlango wa moyo wa mshipa mkubwa wa damu iendayo kwenye mapafu kwa kutumia chumba cha moyo cha juu kulia, kutoa dawa ya kuzuia maumivu sehemu ya uti wa mgongo wakati wa upasuaji mkubwa wa moyo”, alisema Dkt. Kisenge.
Mkurugenzi Mtendaji huyo ambaye pia ni Daktari Bingwa wa moyo na mishipa ya damu alisema kupitia mtambo wa Cathlab ambao ni maabara ya uchunguzi wa matatizo na tiba ya magonjwa ya moyo inayotumia mionzi maalumu, wagonjwa 6,260 walipata huduma ya matibabu ambapo kati yao watu wazima walikuwa 5,693 na watoto 567.
Wagonjwa hao walipata huduma za uchunguzi, matibabu ya mishipa ya damu ya moyo iliyokuwa imeziba na kuwekewa vifaa visaidizi vya moyo. Wagonjwa 401 walitibiwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo kwa kutumia mtambo wa kawaida na 81 walitibiwa kwa kutumia mtambo wa Carto 3.
“Matibabu mapya yaliyofanyika katika mtambo wa Cathlab ni pamoja na upasuaji mdogo wa moyo wa kubadilisha valvu ya mshipa mkubwa wa damu bila kufungua kifua (Transcatheter Aortic Valve Implantation procedure – TAVI), kutanua valvu za moyo kwa muda, uchunguzi na kufanya upasuaji wa kuzibua mishipa ya damu ya miguu (Peripheral Interventions) ambayo haipitishi damu vizuri na kuzibua mishipa ya damu ya shingoni”, alisema Dkt. Kisenge.
Akizungumzia kuhusu huduma za tiba mkoba zijulikanazo kwa jina la Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Outreach Services, Dkt. Kisenge alisema zimeshatolewa katika mikoa 13 ambapo watu 11,254 walifanyiwa uchunguzi wa magonjwa ya moyo. Kati ya hao 4,643 walikutwa na matatizo mbalimbali ya moyo na kuanzishiwa matibabu. Wagonjwa 1,378 walikutwa na matatizo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa walipewa rufaa ya kwenda JKCI kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi.
Wataaamu wa Taasisi hiyo pia walivuka mipaka ya nchi na kwenda kutoa huduma za matibabu ya moyo katika nchi za Zambia na Malawi kwa wagonjwa 731.