Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wadau Wajadili Mtaala wa Mafunzo kwa Vyuo vya Ustawi
Jan 18, 2018
Na Msemaji Mkuu

Kamishna Msaidizi Ustawi wa Jamii (Mafunzo) kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Bw. Simon Panga amesema utengenezaji mitaala ya taaluma ya Ustawi wa Jamii katika ngazi ya stashahada na astashahada itasaidia kuboresha elimu ya ustawi wa jamii nchini.

Panga alisema hayo leo wakati akifungua mkutano wa siku moja wa wadau wa Ustawi wa Jamii kutengeneza mtaala wa Ustawi wa jamii kwa vyuo vinavyofundisha masuala ya Ustawi katika ngazi ya stashahada na astashahada leo jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Kamishna Panga, mtaala utakaopendekezwa  na wadau utatumika na vyuo vyote nchini tofauti na sasa ambapo kila chuo kinajitengenezea mtaala na utakuwa umepunguza majukumu na gharama kwa vyuo katika kutengeneza na kuandaa mitaala yao.

Alisema, mtaala pendekezwa unaoanzia ngazi ya stashahada na astashahada utasaidia kuzalisha maafisa ustawi wa jamii wenye sifa stahiki zitakazowawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi hasa ikizingatiwa kumekuwa na changamoto nyingi katika masuala ya kiuchumi na kijamii hasa katika masuala ya utumiaji dawa za kulevya, unyanyasaji wa kijinsia na kadhalika.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Paulo Mwangosi alisema lengo la kuwashirikisha wadau katika mkutano wa kukutengeneza mtaala kwa vyuo vinavyotoa elimu ya  Ustawi wa jamii ni kuja na mtaala shirikishi utakaotumika na vyuo vyote vya Tanzania  ambapo kwa sasa kumekuwa na vyuo vingi na kila chuo kina mtaala wake.

Kwa mujibu wa Mwangosi, kutokuwepo mtaala mmoja unaotumika na vyuo vinavyotoa elimu ya Ustawi wa jamii kunaleta mkanganyiko katika dhana nzima ya utoaji elimu hiyo kwa wanafunzi na kusisitiza kuwa elimu ya ustawi inayotolewa ni lazima ilingane na masuala ya ustawi wa jamii tofauti na ilivyo sasa ambapo  baadhi ya vyuo hutoa elimu hiyo na kuchanganya na mafunzo mengine.

Kwa sasa Tanzania kuna vyuo kumi na saba vinavyotoa mafunzo ya Ustawi wa Jamii na kati ya vyuo hivyo vyuo kumi na tano viko Tanzania bara na vyuo viwili viko Zanzibar.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi