Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uwanja wa Ndege Dodoma Huduma Saa 24 Kuanzia Oktoba 2023
Sep 08, 2023
Uwanja wa Ndege Dodoma Huduma Saa 24 Kuanzia Oktoba 2023
Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara yake ya kukagua hatua iliyofikiwa katika uwekaji wa mfumo wa taa za kuongezea ndege kutua na kuruka.
Na Frank Mvungi

Ndege zinatarajia kuanza kutua kwa saa 24 katika uwanja wa ndege wa Dodoma kuanzia Oktoba 2023.

Hayo yamesemwa leo Septemba 8, 2023 na Waziri wa Uchukuzi Mhe. Prof. Makame Mnyaa Mbarawa wakati wa ziara yake ya kukagua hatua iliyofikiwa katika uwekaji wa mfumo wa taa za kuongezea ndege kutua na kuruka.

"Mradi huu wenye thamani takribani shilingi bilioni 8 za kitanzania unaleta mageuzi makubwa katika utoaji wa huduma katika uwanja wa ndege Dodoma," alisisitiza Prof. Mbarawa

Akieleza zaidi, amesema kuwepo kwa mfumo wa taa katika uwanja huo utawezesha kuongezeka kwa safari za ndege kuja na kutoka katika jiji la Dodoma kutoka wastani wa safari 4 hadi 10 kwa siku.

Aidha, alibainisha kuwa, dhamira ya Serikali kwa sasa katika ujenzi wa viwanja vya ndege hapa nchini ni kuhakikisha kuwa vinakuwa na mfumo wa kisasa wa umeme unaowezesha ndege kuruka na kutua kwa saa 24.

Kuwekwa mfumo huo wa kisasa wa taa za kuongezea ndege utachochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa huduma za Uhandisi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) Bw. Focus Kadeghe amesema kuwa mfumo huo utawezesha uwanja huo kuwa umeme wa uhakika kwa kuwa mifumo yake inawezesha uwanja huo kutunza umeme wa akiba kwa zaidi ya saa 8 kuanzia umeme unapokatika.

Aidha, aliongeza kuwa mradi huo umefikia zaidi ya asilimia 90 na unatarajiwa kukamilia Septemba 15, 2023, na kubainisha kuwa mfumo wa taa hizo ni wa kisasa na utaongeza tija katika utoaji huduma katika uwanja huo.

Naye Meneja wa uwanja huo Bi. Betha Bankwa amesema, mahitaji ya watoa huduma ni mengi na kuwekwa kwa mfumo huo unaowezesha uwanja huo kutoa huduma kwa saa 24.

Sanjari na hilo, aliwakaribisha watoa huduma wote kwa kuwa wamejipanga kutoa huduma kwa saa 24 na majaribio ya utaratibu huo yalishaanza.

Viwanja vingine vyenye mfumo wa kisasa wa umeme unaowezesha ndege kuruka na kutua kwa saa 24 ni pamoja na, KIA, Zanzibar, Songwe na JNIA.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi