Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania hususan wanasiasa kuzingatia maadili na taratibu za nchi katika kutumia uhuru wa kutoa maoni ambao Serikali imeutoa kwa kila Mtanzania.
Rais Samia amesema hayo leo Septemba 11, 2023 wakati akifungua Mkutano Maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa unaoshirikisha Wadau wa Demokrasia ya Vyama Vingi vya Siasa, kutathmini utekelezaji wa Mapendekezo ya Kikosi Kazi na Kujadili hali ya Siasa Nchini katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano JNICC, Dar es Salaam.
Rais Samia alisema kila nchi ina mambo yake na kwamba Demokrasia ni jinsi nchi inavyoendesha masuala yake na si kuiga za nchi zingine na kulazimisha kubadili mienendo ya Tanzania na kuwakumbusha wanasiasa misingi ya kufuatwa ambayo ni pamoja na kuheshimu maazimio, sheria za Serikali, kuheshimiana.
“Marekebisho ya Katiba yetu yameanza kufanyiwa kazi, si mali ya vyama vya siasa bali ni mali ya Watanzania wote, hatutakurupuka katika hili, tutaenda taratibu ili kuweka kila kitu sawa ikiwemo kutoa elimu kwa Watanzania ili kila mtu atoe maoni yake ya nini kibadilike,” alisema Rais Samia.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa alisema kisiasa nchini inaendelea vizuri na kwamba mahusiano ya vyama yanazidi kuimarika na Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo imepewa dhamana ya kuratibu shughuli za kisiasa inaendelea kushirikiana na vyama vyote kupitia Baraza la Vyama vya Siasa nchini.
“Mheshimiwa Rais, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Makamu wa Rais Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mawaziri wa nchi wa ofisi hizi wameendelea kuratibu hatua kwa hatua mpaka kuunda vikosi kazi ambavyo vimeendelea kufanya jukumu hili na hatimae kuifikia hatua ya kuwa na m pango mkakati wa namna ya kwenda ili kuimraisha mwenendo wa vyama hapa nchini,” alisema Mhe. Majaliwa.