Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TFRA Yatekeleza Agizo la Rais Kusambaza Mbolea Nchi Nzima
Jan 11, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Fatma Salum.

Kufuatia agizo la Mhe. Rais John Pombe Magufuli la kuwataka watendaji wanaohusika na usambazaji wa mbolea nchini kukamilisha kazi hiyo kabla ya Ijumaa wiki hii, zaidi ya nusu ya mbolea hiyo tayari imesambazwa nchi nzima.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) Bw. Lazaro Kitandu ameiambia Idara ya Habari (MAELEZO) kuwa hadi kufikia leo tayari zaidi ya nusu ya mahitaji ya mbolea inayohitajika imeishasambazwa katika mikoa yote nchini na kazi ya usambazaji bado inaendelea.

“Hadi kufikia leo jumla ya tani 118,613 za mbolea zimesambazwa katika mikoa yote nchini ikiwemo mikoa ambayo ina uhaba mkubwa wa mbolea.  Akiba iliyopo ni tani 114,477 kwa mbolea za aina zote zikiwemo tani 28,000 za UREA ambazo zinaendelea kusambazwa,” alifafanua Kitandu.

Kitandu alieleza kuwa mbolea tayari imefika kwenye maeneo yote yaliokuwa na upungufu ikiwemo mikoa ya Rukwa na Ruvuma na amewahakikishia wananchi kuendelea kupata mbolea za aina zote kwa matumizi ya msimu huu.

“Kwa siku mbili za Jumanne na Jumatano gari za jeshi zenye tani 500 za mbolea zilienda mkoani Rukwa na zaidi ya tani 1,200 zilipelekwa kwa kutumia magari ya makampuni ya watu binafsi,” alisema Kitandu.

Aliongeza kuwa katika mkoa wa Katavi pia kulikuwa na uhaba wa mbolea ya kukuzia aina ya CAN lakini kwa sasa mbolea hiyo pamoja na ile ya UREA zenye jumla ya tani 400 tayari zimekwisha pelekwa.

Aidha, Kitandu alieleza kuwa mikoa ya nyanda za juu kusini hutumia takriban asilimia 60 ya mbolea zote zinazotumika nchini ambapo mbolea ya UREA hutumika kwa wastani wa tani 3,500 hadi tani 10,000 kwa kila mkoa kila mwaka huku mkoa wa Njombe ukiwa na matumizi makubwa zaidi.

Jumla ya mbolea zinazotumika nchini ni tani 200,000 ambapo kufikia Disemba mwaka jana ziliingizwa nchini jumla ya tani 233,090 zikiwemo mbolea za kupandia za Minjingu, DAP, TSP, MOP na NPK, na mbolea za kukuzia aina ya UREA, CAN na SA.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi