Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Yashiriki Maonesho ya 68 ya Vito Thailand
Sep 06, 2023
Tanzania Yashiriki Maonesho ya 68 ya Vito Thailand
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Maonesho ya 68 ya Vito na Usonara katika jiji la Bangkok nchini Thailand
Na Wizara ya Madini - Bangkok

Ushiriki wa Tanzania katika Maonesho ya 68 ya Vito na Usonara katika jiji la Bangkok nchini Thailand, umewavutia wafanyabiashara mbalimbali wa madini kutokana na wengi kutumia malighafi za madini kutoka nchini.

Akizungumza baada ya kushiriki hafla fupi ya ufunguzi wa maonesho hayo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya  Madini, Msafiri Mbibo amesema  wafanyabiashara wakubwa wa madini nchini humo wakiwemo viongozi wa Serikali wameonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika nyanja mbalimbali zikiwemo  biashara ya madini, uongezaji thamani madini pamoja na kubadilishana uzoefu katika shughuli hizo.

“Uwepo wa Tanzania katika maonesho haya ya madini yenye thamani kubwa unalenga kujifunza pamoja na kuhamasisha urejeshwaji wa minada ya madini nchini na kuhamasisha uwepo wa masoko ya madini ambapo wafanyabiashara wanaweza kununua madini kupitia masoko ya madini yaliyoanzishwa katika kila mkoa nchini”, anaeleza Mbibo.

Ameongeza kuwa, tayari Serikali ya Awamu ya Sita imefungua milango  ya biashara katika Sekta ya Madini na kuwataka wadau wa madini nchini kutumia fursa hiyo kuwapokea wawekezaji mbalimbali  ili hatimaye  kujenga uchumi imara na kuinua ustawi wa watanzania  kupitia rasilimali madini.

Akizungumza baada ya ujumbe wa Tanzania kutembelea banda la Kampuni ya  Bright Future katika maonesho hayo, Mkurugenzi wa Kampuni  hiyo Ashish Baid ambaye pia   ni Makamu wa Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Madini nchini humo  na mfanyabiashara wa madini ya Tanzanite na madini  mengine, ameelezea nia yake ya dhati kupitia jukwaa hilo na kampuni yake binafsi  ya kushirikiana na Tanzania katika kuipa  thamani ya kimataifa  minada ya madini  endapo Serikali itakuwa yatari kushirikiana  nao ikiwemo katika eneo la uongezaji thamani madini.

Naye, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Fine Gamestone  Sukharit Sinchawla   amesema amefurahishwa na uwepo wa Tanzania katika maonesho hayo na kusema ni nchi nzuri  yenye madini  mengi mazuri na yenye thamani kubwa  na kueleza kwamba ni nchi ambayo kampuni yake inatumia  madini mengi kufanya biashara yakiwemo ya Spinel  na Tanzanite.


Wadau muhimu wapatao 31 elfu kutoka maeneo mbalimbali duniani wanatarajia kutembelea maonesho hayo   kutoka nchi 21   na waoneshaji takribani 1,100. Maonesho ya BangKok yanatajwa kuwa maonesho makubwa na ya kuaminika ambayo wafanyabiashara wachimbaji wanaweza kuyatumia kujenga uhusiano wa kibiashara, kutangaza bidhaa zao na kuuza.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi