Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania Yang'ara Sekta ya Viwanda
Sep 20, 2023
Tanzania Yang'ara Sekta ya  Viwanda
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia na viongozi wengine wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa kiwanda cha vifaa vya ujenzi (Sapphire Float Glass Tanzania) chenye thamani ya Dola za Marekani milioni 311 kilichopo Mkuranga mkoani Pwani.
Na Immaculate Makilika - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia amefungua kiwanda cha vifaa vya ujenzi (Sapphire Float Glass Tanzania), chenye thamani ya dola za Marekani milioni 311.

Akizungumza wakati anafungua kiwanda hicho leo Mkuranga, mkoani Pwani  amesema kuwa tukio hilo ni muhimu  kwa sekta ya viwanda na uwekezaji nchini, na kuwa  uanzishwaji wa  viwanda umeendelea  kuongezeka.

"Pwani  ina idadi ya viwanda  1525, Kituo cha Uwekezaji (TIC) hadi kufikia Septemba mwaka huu  imesajili viwanda 417 vyenye  thamani ya shilingi trilioni 12", amesema Rais Samia.

Kuhusu  bidhaa zinazozalishwa  katika kiwanda hicho, Rais Samia amesema kuwa asimilia 75 ya bidhaa  zitauzwa nje ya nchi na asilimia  25  nchini.

Aidha, Mhe. Rais Samia amesema kuwa Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na tayari  imefanya maboresho mengi ya kisera na kanuni ili uwekezaji kuwa na mazingira bora. Pia,  mwaka 2022 imerekebisha kanuni ili kufanya uwekezaji kuwa na tija zaidi.

Ameongeza, "Serikali inaendelea kuwekeza  kwenye mifumo ya utoaji huduma, ili kurahisisha  usajili na kutoa huduma kwa wawekezaji. Napenda kutumia fursa hii kuyahakikishia makampuni yote yaliyowekeza nchini kuwa mali zao ziko salama".

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji, amesema kuwa mradi huo unatarajia kuingiza nchini fedha za kigeni milioni 180 kwa mwaka.

"Hapa zimepatikana  ajira 750, kiwanda hiki kikikamilika zitapatikana ajira 1650. Vilevile, tunao uwezo wa kuhakikisha asimilia 100 ya malighafi zinazohitajika zinapatikana Tanzania", ameeleza Waziri Kijaji.

Amefafanua kuwa kiwanda hicho kinatumia madini ya soda ash na chuma ambayo yanachukuliwa nje ya nchi, licha ya  kuwa madini hayo yanapatikana nchini.

"Tumeanza mazungumzo na kiwanda hiki ili asilimia 100 ya malighafi zinazohitajika zipatikane ndani ya nchi", amebainisha Waziri Kijaji.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Wangkang  Investment Group, Bw. Frank Yang amesema kuwa kiwanda hicho ni cha nne kwa ukubwa katika Bara la Afrika na  wateja wa bidhaa zao wanatoka ndani ya nchi za Jumuiya Afrika Mashariki na SADC.

"Umuhimu wa mradi huu ni kuhakikisha Tanzania inaongeza uzalishaji wa bidhaa zinazotengenezwa kwa kioo  pamoja na kukuza ushirikiano wa Tanzania na China.

Aidha, Mhe. Rais Samia amehitimisha ziara yake kwa kufungua  kiwanda cha vifaa vya ujenzi katika Mkoa wa Pwani.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi