Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli akiwaeleza baadhi ya Viongozi mbalimbali Waandamizi wa Serikali ya Tanzania, Misri na Waandishi wa Habari kuhusu makubaliano mbalimbali waliyofikia kati ya Serikali ya Tanzania na Misri mara baada ya kumaliza mazungumzo na Mgeni wake Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah Al Sisi, leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Na. Said Ameir-MAELEZO
Rais John Pombe Magufuli na Rais Abdel Fattah Al Sisi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri wameahidi kuongeza nguvu katika kuimarisha na kuendeleza uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya nchi zao.
Wakizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar Es Salaam leo mara baada ya kuongoza mkutano wa mashauriano kati ya Serikali za Tanzania na Misri, viongozi hao walisema kuwa katika mkutano huo pande mbili hizo zimekubaliana kuchukua hatua za haraka ili kuongeza kasi ya uhusiano na ushirikiano.
“Tumekubaliana kuongeza kasi ya uhusiano na ushirikiano wetu na katika kutekeleza hilo tumeamua kufufua Kamisheni ya Ushirikiano kati ya nchi zetu na kuagiza mikutano hiyo ya mashaurisno ifanyike kwa haraka”Rais Magufuli alieleza.
Rais wa Misri Abdel Fattah Al Sisi akizungumza na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Tanzania na Misri pamoja na Waandishi wa Habari mara baada ya kumaliza mazungumzo ya ndani na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
Alieleza kuwa Kamisheni hiyo ambayo ndio inayoratibu na kuongoza mashirikiano kati ya nchi hizo ilikutana kwa mara ya mwishio miaka 20 iliyopita hivyo kupunguza kasi ya mashirikiano katika baadhi ya maeneo.
Aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Serikali hizo nimedhamiria kuimarisha uhusiano kati yao ikiwa ni sehemu ya kuienzi historia nzuri ya ushirikiano iliyoasisiwa na Rais Julius Nyerere na Gamal Abdel Nasser.
Katika mnasaba huo, nchi hizo zimekubaliana kuongeza ushirikiano katika maeneo yanayoshirikiana sasa na kuangalia maeneo mengine zaidi kwa manufaa ya Serikali na wananchi wa pande zote mbili.
Rais Magufuli aliyataja mambo mengine waliyokubaliana kuwa ni pamoja na kupanua biashara na uwekezaji, kilimo, elimu, afya pamoja na ulinzi na usalama.Alibanisha kuwa chini ya makubaliano hayo, Misri itaanzisha kiwanda kikubwa na kisasa cha nyama humu nchini ili nchi hiyo iweze kukidhi mahitaji yake ya nyama pamoja na kuuza katika masoko ya nje.
Halikadhalika, Misri imeahidi kupanua wigo wa misaada yake kwa Tanzania katika sekta za afya na elimu ambapo kwa upande wa afya nchi hiyo itaijengea uwezo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili iweze kufanya upasuaji wa figo ifikapo mwaka 2020.
Kwa upande wa elimu, Rais Magufuli alibainisha kuwa nchi hiyo imekubali kuongeza nafasi za masomo kwa vijana wa Tanzania ambapo alieleza kuwa kwa sasa watanzania 115 wako nchini humo wakichukua mafunzo katika fani mbali mbali.
Baadhi ya Viongozi mbalimbali Waandamizi wa Serikali ya Tanzania na Misri na Waandishi wa Habari wakimsikiliza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli wakati akielezea makubaliano mbalimbali waliyofikia kati ya Serikali ya Tanzania na Misri mara baada ya kumaliza mazungumzo na Mgeni wake Rais wa Misri Mhe. Abdel Fattah Al Sisi, leo Ikulu jijini Dar es Salaam.
(Picha na Eliphace Marwa –MAELEZO)