Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TAMISEMI,Wataalam Sekta ya Ardhi Watakiwa Kujipanga Kutatua Changamoto za Ardhi
Oct 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Anthony Ishengoma na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angeline Mabula amewataka wakurugenzi wa Halmashauri nchini kujipanga na kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu wa ardhi ili kuondoa changamoto zinazojitokeza katika utendaji kazi na usimamizi wa sekta ya ardhi katika Halmashauri.

Dkt. Mabula alisema hayo leo Oktoba 1, 2022 wakati wa ufunguzi wa kikao kazi kilichowaunganisha Wakurugenzi wa Halmashauri na watalaam wa Sekta ya Ardhi nchini kilichofanyika jijini Dodoma. Kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kupata maoni juu ya muundo mpya wa utendaji kazi wa wataalam wa ardhi katika ngazi ya Halmashauri.

Dkt. Mabula alisema, zimeanza kujitokeza changamoto katika utendaji kazi kati ya watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa Halmashauri  hasa katika eneo la usimamizi wa sekta hiyo baada ya kuanza utekelezaji wa rejesho la Waraka wa Utumishi Na 1 wa Mwaka 1998 kuhusu usimamizi wa watumishi wa sekta ya ardhi na maji kutokana na sababu mbalimbali.

Rejesho hilo pamoja na mambo mengine liliwahamisha wataalamu wa sekta ya ardhi kutoka kwenye usimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kiajira na kinidhamu na kuwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Ardhi.

 ‘’Watumishi hawa kiajira na kinidhamu wako Wizara ya ardhi, mamlaka za upangaji ardhi ziko Halmashauri lakini baadhi ya Wakurugenzi wamekuwa wakijiweka mbali na wataalam ardhi na kushindwa kufuatilia utekelezaji wa sekta ya ardhi au kukosa ufahamu katika sekta ya ardhi.’’ Alisisitiza Dkt. Mabula

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula changamoto hiyo imeleta mkanganyiko kwa kuwa baadhi ya watendaji hasa Wakurugenzi hawaoni kama wana wajibu wa kusimamia sekta ya ardhi wakati wao ni mamlaka za upangaji ardhi.

‘’Baadhi ya Wakurugenzi hawajui taratibu za ardhi na kutojihusisha zaidi na uelewa wa masuala ya ardhi kwani unakuta Mkurugenzi wa Halmashauri ukimtaka akupe taarifa anakimbilia kupata ufafanuzi kutoka kwa mtaalamu wa ardhi’,’Aliongeza Dkt. Angeline Mabula.

Changamoto nyingine iliyobainishwa na Dkt Mabula ni kitendo cha baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri kushindwa kurejesha fedha za mkopo wa program ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi na kutumia fedha hizo kwenye mipango mingine badala ya kurejesha fedha hizo ili ziweze kutumika katika maeneo mengine.   

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Allan Kijazi alieleza kupitia kikao hicho kuwa ipo haja ya kuboresha mawasiliano kati ya watendaji wa sekta ya adhi na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuweka mkakati mzuri wa utendaji kazi kwani wote ni watumishi wa Serikali.

Dr. Kijazi aliongeza kuwa, kumekuwa na changamoto ya kiutendaji kati ya Serikali za Mitaa na uongozi wa kisiasa ikiwemo Madiwani na kusisitiza kuwa, la msingi ni kufanya kazi kwa pamoja kwa kuwa wote ni Watendaji wa Serikali.

‘’Lengo la kikao chetu ni namna ya kuboresha mawasiliano ili tuweze kujiweka sawa kuboresha utendaji kazi kwani kumekuwa na lugha zinazoleta sintofahamu kuwa baadhi ya Wakurugenzi wa Halmashauri wamekuwa wakitoa kauli kuwa watendaji wa sekta ya ardhi wako chini ya katibu Mkuu na wao hawahusiki’’. Alisema Dkt. Kijazi

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi