Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Taarifa kwa Umma
Jul 05, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 5 Julai 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambaye ni Mratibu wa Mpango wa Ushirikiano katika Usambazaji wa Chanjo ya Uviko19 Mhe. Ted Chaiban, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam.

Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amesema Serikali imelenga kushirikiana na jumuiya ya kimataifa katika kukabiliana na Uviko 19 ikiwemo kutoa chanjo hususani kwa watu wote walio katika hatari ya kupata madhara zaidi ya ugonjwa huo. 
Amesema katika kudhibiti ugonjwa huo, Tanzania imeendelea kuimarisha mifumo ya afya, kuwajengea uwezo watumishi wa Afya katika kukabiliana na ugonjwa huo, kuimarisha huduma za dharura pamoja na ujenzi na ukarabati wa vituo vya afya ili kusaidia huduma muhimu ya afya ambayo iliathiriwa na janga la Uviko 19 hususani kwa huduma ya afya ya msingi.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba pamoja na mafaniko yaliyopatikana katika kudhibiti Uviko 19 bado Serikali inaendelea kuchukua hatua muhimu katika kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na  kujenga miundombinu itakayoweza kukabiliana na magonjwa ya mlipuko pindi yatakapotokea.
Kwa upande wake Mratibu wa Mpango wa Ushirikiano katika Usambazaji wa Chanjo ya Uviko 19 Mhe. Ted Chaiban, ameipongeza Tanzania kwa juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa idadi ya utoaji wa chanjo. Amesema ofisi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuwafikia watu wengi zaidi wanaohitajika kupata chanjo ikiwemo makundi maalum kama vile watumishi wa afya pamoja na wazee.
Aidha, amesema juhudi za ufanikishaji wa utoaji chanjo zinapaswa kuhusisha moja kwa moja ngazi ya mikoa na wilaya ili kufikia kirahisi malengo ya taifa katika zoezi hilo. Pia Chaiban amesema kwamba ipo haja ya kuwaelimisha watumishi wa sekta muhimu kama vile Elimu na Utalii ili kuendelea kuhamasisha zoezi la upokeaji chanjo katika sekta zao.
Amesema changamoto za Uviko 19 zinatoa funzo kwa mataifa hususani yanayoendelea kuwekeza katika afya ya msingi pamoja na kuongeza uzalishaji wa ndani ili kuendelea kupata bidhaa hususani wakati wa mlipuko wa magonjwa duniani. 
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi