Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

SIDO Yaanzisha Mkakati wa Wilaya Moja Bidhaa Moja
Jul 10, 2017
Na Msemaji Mkuu

Frank Mvungi

Katika Kuhamasisha Ujenzi wa Uchumi wa Viwanda, Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) limeanzisha Mkakati wa Wilaya Moja Bidhaa Moja (ODOP) ili kuchochea maendeleo ya Viwanda vidogo kwa lengo la kuongeza kipato na ajira kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa maonesho ya 41 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam, Afisa Mwandamizi Uendelezaji Biashara wa SIDO Bw. Stephen Bondo amesema dhamira ya Shirika hilo ni kuhakikisha kuwa kuna viwanda katika Halmashuri zote kwa kufuata mpango wa Wilaya moja Bidhaa moja.

“Mkakati huu unakusudia kuibua na kuendeleza bidhaa moja kwa awamu katika Wilaya kwa kuzingatia rasilimali zilizopo katika Wilaya husika kwa kuhakikisha kuwa wadau wanachagua na kuwekeza katika viwanda vidogo na kuzalisha bidhaa ili kuweza kuharakisha maendeleo ya kiuchumi Vijiji,” alisisitiza Bondo.

Bondo lifafanua kwa kusema kuwa nchi ya Japan imefanikiwa katika sekta ya viwanda kwa kutumia mfumo huo ambao umeteklezwa katika Taifa hilo hadi ngazi ya Vijiji na kuchochea maendeleo yanayoonekana leo hii katika Taifa hilo.

Akizungumzia malengo ya ODOP, Bondo amesema kuwa ni pamoja na kutumia rasilimali au malighafi, utaalamu na ujuzi unaopatikana katika Wilaya husika na kuwawezesha wale wanaotaka kuanzisha viwanda kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa katika Wilaya husika hadi kufikia kuwa bidhaa.

Aliongeza kuwa eneo jingine la utekelzaji wa mpango huo ni kujenga uwezo kwa wajasiriamali vijijini katika mbinu za kibiashara na teknolojia ili kuweza kushindana katika soko la Wilaya, Mkoa, Taifa na Kimataifa.

Pia kujenga mahusiano ya Viwanda vidogo na vikubwa kwa viwanda vikubwa kuwa na mikataba ya kuboresha na kutumia bidhaa za viwanda vidogo ili kupanua soko la viwanda vidogo.

Kwa upande wake Meneja Masoko wa SIDO Bi. Lilian Masawe amesema wanachi wajitokeze katika Wilaya zao kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuanzisha viwanda katika maeneo yao kwa kuwa malighafi zipo na SIDO iko tayari kusaidia.

Alitaja baadhi ya Wilaya zilizofanikiwa kutekeleza mpango huo kwa kushirikiana na wadau kuwa ni Geita, Longido,Monduli,Singida na Wilaya zote hapa nchini kwa kuwa mpango huo unatekelezwa katika Mikoa yote, dhamira ikiwa ni kujenga Tanzania ya viwanda kuanzia ngazi ya Wilaya,Vijiji , Mikoa na Taifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi