Tanzania imeendelea kupiga hatua katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu, kwa utashi thabiti wa kisiasa na dira ya kuifanya Tanzania kuwa taifa linalojegwa kwa kutumia sayansi na teknolojia.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu, Tume ya Taifa na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu leo Machi 17, 2025 katika ofisi za Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma wakati wa mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa tume hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, serikali imewekeza shilingi bilioni 25.7 katika utafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH),” amesema Dkt. Nungu.
Amesema hatua hiyo si tu kwamba imeendelea kuimarisha msingi wa maendeleo ya kisayansi, bali pia imethibitisha dhamira ya serikali ya kujenga taifa linalowekeza katika kuibua teknolojia, likiongozwa na tafiti na ubunifu.
Aidha, serikali kupitia COSTECH, imefadhili zaidi ya tafiti 50 katika sekta za elimu, kilimo, afya na mazingira ili kuhakikisha maarifa haya yanatumika kuboresha maisha ya Watanzania.
“Zaidi ya vituo vya ubunifu 111 vimeimarishwa, huku tafiti zikibadilika kuwa suluhisho za kisayansi kwa jamii. Vilevile kampuni mpya zipatazo 70 zimesajiliwa ikiwa ni matokea ya wabunifu waliyowezeshwa na serikali,” amefafanua Dkt. Nungu.