Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yaanza Kutumia Ndege Kulinda Misitu
Sep 14, 2018
Na Msemaji Mkuu

Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), imeanza kutumia safari za anga kufanya doria katika kukabiliana na changamoto kubwa inayoikabili serikali katika uhifadhi wa Sekta ya misitu na maliasili kwa jumla.

Akizungumza na gazeti hili jana jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa TFS, Professa Dos Santos Silayo amesema lengo la doria hizo ni kuhakikisha ulizi unaimarishwa katika maeneo yote ya misitu ambayo TFS imepewa dhamana ya kuilinda.

“Nimeelekeza watendaji wangu kufanya doria ya anga kuanzia leo na tutaanza na Kanda ya Mashariki na nizitake kanda nyingine zijipange, maeneo/misitu korofi myabaini na kutafuta ramani zake. Nitawatumia ndege kwa ajili ya doria kutambua uharibifu.

“Tumekuwa tukifanya doria za misitu lakini tumekuwa tukiwiwa vigumu kuyafikia maeneo yote, lakini kupitia doria za anga sasa tutajua kila kinachoendelea kwenye eneo la misitu na kwa kutumia vikosi kazi vyetu tutafanya ulinzi kwa uhakika zaidi,” amesema Profesa Silayo.

Professa Silayo aliongeza kuwa ili kuongeza tija TFS itashirikiana na Wakuu wa wilaya pamoja wa wataalamu wa ardhi wa maeneo husika.

Akizungumzia mara baada ya kufanya doria ya anga, Meneja Msaidizi wa TFS, Kanda ya Mashariki, Bernadetha Kadala alisema doria hio imewawezesha kuona kwa karibu zaidi hali halisi ya misitu iliyopo kwenye Kanda za Mashariki na kufahamu kuna nini kinachotokea kwa wakati huo na hivyo itawawezesha kufanya ulinzi kwa weledi.

“Leo tumeangalia misitu kumi (10) iliyopo katika Wilaya ya Rufiji, Kibiti na Mkuranga, tumeweza kubaini mambo kadhaa yanayofanyika kinyume na taratibu na tumechukua kodineti zitakazotuwezesha kufika moja kwa moja katika eneo husika kwa hatua zaidi,” anasema Kadala.

Kadala aliitaja misitu hiyo kuwa ni Mohoro River, Mohoro, Tamburua, Namakutwa/Namueti, Kuchi hills, Kiwengoma na Utete kutoka Wilaya ya Rufiji huku misitu ya Wilaya ya Kibiti ikiwa ni Rufiji delta na Mchungu, na Wilaya ya Mkuranga walitembelea Msitu wa Masanganya.

Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Filberto Sanga aliyekuwepo kwenye doria hiyo anasema, wilaya yake inaendelea na zoezi la kuwaondoa wafugaji waliovamia misitu iliyohifadhiwa lakini kupitia doria hio amebaini wafugaji wanashirikiana kukwamisha zoezi la kuwaondoa msituni.

Sanga anasema kupitia doria hio amebaini kuwepo kwa ng’ombe wengi katikati ya kijiji ikiwa na maana kwamba wameondolewa msituni na kufichwa kijijini kwa kuwa aliwatarifu kuwepo kwa operesheni hio; na kuahidi kupanga mikakati madhubuti itakayowezesha kumaliza kabisa tatizo la wafugaji wanaohamahama.

Sekta ya misitu na maliasili kwa jumla zina kukabiliwa na changamoto kubwa katika uhifadhi, kutokana na kubadilika kwa mazingira ya kazi na mifumo ya kihalifu yanayosababisha mfumo wa utendaji wa sasa wa TFS kujikita zaidi katika matumizi ya tekinolojia na vifaa vya kisasa zaidi kuhakikisha uwepo wa usimamizi madhubuti na wenye ufanisi na tija wa rasilimali za misitu na nyuki.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi