Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali ya Ujerumani Yaomba Radhi Vita ya Majimaji
Nov 01, 2023
Serikali ya Ujerumani Yaomba Radhi Vita ya Majimaji
Rais wa Ujerumani, Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier akitoa heshima katika moja ya kaburi la wanajeshi waliopigana vita ya maji maji wakati alipotembelea Makumbusho ya Kumbukumbu ya Vita vya Majimaji Songea mkoani Ruvuma leo Novemba 1, 2023
Na John Mapepele

Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani imeiomba radhi Tanzania kwa makosa ya ukatili na mauaji yaliyofanywa ya wanajeshi wa nchi hiyo wakati wa vita ya majimaji na kutaka  kufanyika  mazungumzo  baina ya  serikali hiyo ili kutumia suala hilo kuimarisha  mahusiano  kwa faida  ya nchi zote mbili.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Ujerumani, Mhe. Dkt. Frank-Walter Steinmeier aliyetembelea Makumbusho ya Kumbukumbu ya Vita vya Majimaji Songea mkoani Ruvuma leo Novemba 1, 2023 ambapo pia amezungumza na baadhi ya ndugu wa marehemu mashujaa wa vita hiyo na hatimaye  kutoa katika makaburi yaliyopo katika makumbusho hayo.

“Nimeguswa sana, ninaona aibu kwa majeshi ya wajerumani waliyowatendea, lakini licha ya historia hii ninaomba msamaha kwa mambo waliyoyatenda,” amesisitiza Rais Steinmeier

Aidha, amesema Serikali yake ipo tayari kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania kuyapatia majibu maswali yote  yanayohusiana na suala  hilo kwa faida ya pande zote mbili.

Naye Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dustan Kitandula amesema historia ya uhifadhi Tanzania haiwezi kuandikwa na kukamilika bila kutaja juhudi zilizofanywa na utawala wa Kijerumani katika koloni la Tanganyika kwa kuasisi utafiti na uhifadhi wa kisasa wa maliasili na malikale ambapo mwaka 1896 kuliandaliwa sheria na kanuni za utafiti wa mila na palentolojia.

Amesema utafiti huo baadaye ulibaini kuwepo kwa masalia ya binadamu wa kale (jamii ya Zinjanthropus boisie) katika Bonde la Olduvai ambapo pia utafiti huo pamoja na faida nyingine, uliithibitishia dunia kuwa Tanzania ndiyo chimbuko la binadamu.

Amefafanua kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii inathamini sana mchango ambao Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani imekuwa ikitoa katika nyanja za sekta ya maliasili na malikale kupitia mafunzo, kubadilishana uzoefu na utafiti wa pamoja.

“Mathalan mwaka 2005, wakati wa kumbukumbu za miaka 100 ya Vita ya Majimaji, Ubalozi wa Ujerumani nchini ulifadhili utafiti uliowezesha upatikanaji wa baaadhi ya taarifa na vioneshwa ambavyo muda uliopita umeviona ndani ya ukumbi wa historia, amesisitiza Mhe Kitandula.

Ameongeza kuwa, wakati tukitambua mchango huo, Wizara ipo tayari kwa majadiliano zaidi ambayo yatalenga kutumia historia ya vita ya Majimaji kwa faida za kijamii na kiuchumi kwa pande zote mbili.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi