Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali ya Tanzania Yakaribisha Wawekezaji Sekta ya Kilimo
Mar 15, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Mwandishi Wetu - Dodoma

Serikali ya Tanzania imewakaribisha Wawekezaji wa masuala ya kilimo kuwekeza nchini ili kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na kuimarisha lishe kwa wananchi na kuinua Pato la Taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge, na Uratibu, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) Tanzania, Bi. Sarah Gibson na Mkurugenzi wa Shirika hilo Kanda ya Kusini wa Afrika, Dkt. Manghestab Haile Ofisini kwake Bungeni Jijini Dodoma.

Akieleza baadhi ya masuala yaliyoafikiwa ni pamoja na kuboresha suala la lishe kwa wananchi licha ya uzalishaji mkubwa wa chakula katika maeneo mbalimbali hatua itakayoboresha afya na kuepuka utapiamlo huku akisema kuwa Tanzania ni sehemu salama kwa ajili ya kufanya uwekezaji katika kilimo.

“Tunaposhirikiana na WFP chini ya Rais wetu mpendwa, Mhe. Samia Suluhu Hassan Tanzania ni eneo sahihi kabisa katika uzalishaji wa chakula, tumekuwa  tukizalisha chakula cha kutosha na tumekuwa mfano ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za SADC na tumekuwa tukipeleka chakula nje ya Nchi,”alisema Mhe. Pindi Chana.

Waziri Pindi alieleza kwamba, wamefikia makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya maafa pindi yanapojitokeza kwani yamekuwa yakisababisha maafa kwa raia kama vifo, mali zao kuharibiwa na miundo mbinu.

Vilevile, Mhe. Pindi alibainisha kwamba wamekubaliana kuboresha suala la kilimo kuendana na teknolojia iliyopo sasa na matumizi sahihi ya pembejeo pamoja na ushirikishwaji wa vijana katika uzalishaji wa chakula, masoko na kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo.

“Katika majadiliano tumezungumzia suala zina la kilimo kuna matumizi ya vitendea kazi vya kisasa, ushirikishwaji wa vijana maana idadi kubwa ya umri wa watu ni vijana kwa hiyo ni jinsi gani tunahamasisha vijana katika uzalishaji wa chakula na kuongeza thamani yake,” alieleza Mhe. Pindi.

Katika hatua nyingine, aliwahakikisha kwamba kuelekea Bunge la bajeti ijayo, sekta ya kilimo imepewa kipaumbele kuhakikisha kinaleta tija na kuona namna ya kushirikiana na WFP kuboresha eneo hilo muhimu la chakula.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa nchini Tanzania (WFP), Bi. Sarah Gibson aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa namna ambavyo imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Taifa linakuwa na chakula cha kutosha na chenye ubora akisisitiza kuendeleza uhusiano baina ya Tanzania na Shirika hilo.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) wa Kanda ya Kusini mwa Afrika, Dkt. Manghestab Haile aliiahidi Serikali ya Tanzania kuendelea kushirikiana na Sekta Binafsi, kuimarisha masoko na lishe bora kwa raia wake.

Akihitimisha, Mkurugenzi Msaidizi wa Menejimenti ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw.Charles Msangi alishukuru ugeni huo wa wadau wa maendeleo na kusema kwamba utasaidia kutatua changamoto zilizopo katika usimamizi wa maafa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi