Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Kutunga Sera za Kuimarisha Uchumi
Apr 21, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Benny Mwaipaja, Washington DC

Waziri wa Fedha na Mipango. Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa Serikali itaendelea kubuni sera zitakazochangia kupunguza makali ya maisha na kuimarisha uchumi ikiwa ni hatua za kupambana na athari za UVIKO 19 na Vita baina ya Urusi na Ukraine.

Dkt. Nchemba alisema hayo Mjini Washington DC nchini Marekani, baada ya kikao cha Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu kutoka Kundi la kwanza la nchi za Afrika, ambazo ni wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Alisema kuwa sera hizo zitalenga kuimarisha sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na kudhibiti mfumuko wa bei za bidhaa zinazotokana na mzozo unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine uliosababisha bei za mafuta ya kula na baadhi ya vyakula na mazao kama ngano kupanda bei kupindukia.

Dkt. Mwigulu alisema kuwa nchi wanachama wa Benki ya Dunia hususan kutoka Bara la Afrika zimeathirika kwa kiasi kikubwa na majanga ya UVIKO 19 pamoja na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine hivyo njia za kukabiliana na hali hiyo zinachukuliwa kwa uzito unaofaa.

“Tumejadiliana hatua za kuchukua kutokana na athari za UVIKO19 na Vita vya Ukraine na Urusi, namna tutakavyokabiliana na madhara ya kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu zinazotumiwa na wananchi wetu ili ziwe nafuu ambapo tumetazama fursa zinazopatikana kupitia Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa-IMF”, alisema Dkt. Nchemba.

Tathimini iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa-(IMF) inaonesha kuwa uchumi wa dunia ulikua kwa wastani wa asilimia 5.9 mwaka 2021 na unatarajiwa kukua kwa asiimia wastani wa 4.9 mwaka 2022.

Katika kukabiliana na UVIKO 19, Benki ya Dunia ilitoa kiasi cha Dola za Marekani bilioni 25.2 ili kuzisaidia nchi wanachama ikiwemo kufadhili program 43 za chanjo ya ugonjwa huo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi