Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Imepoteza Trilioni 108.46 Usafirishaji Makinikia Nje ya Nchi
Jun 12, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_3333" align="aligncenter" width="910"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza wakati wa hafla ya kupokea ripoti ya Kamati Maalum ya Pili ya Uchunguzi wa Madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini sehemu mbalimbali hapa nchini, Ikulu jijini Dar es Salaam leo.(Picha zote na: Frank Shija)[/caption]

Na: Lilian Lundo 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepoteza mapato ya Shilingi Trilioni 108.46 uliosabaishwa na usafirishaji wa mchanga wa dhahabu ‘makinikia’ nje ya nchi katika kipindi cha kuanzia mwaka 1998 hadi mwezi Machi 2017.

Takwimu hiyo imetolewa na Mwenyekiti  wa Kamati ya pili ya kuchunguza usafirishaji wa makinikia nje ya nchi, Profesa Nehemiah Osoro  alipokuwa akiwasilisha taarifa hiyo kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo Ikulu, Jijini Dar es Salaam.

[caption id="attachment_3337" align="aligncenter" width="1000"] Mwenyekiti wa Kamati ya Pili ya iliyoundwa na Rais Magufuli kuchunguza Madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini sehemu mbalimbali hapa nchini Profesa Nehemiah Osoro akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi ripoti yao leo, Ikulu jijini Dar es Salaam. Kutoka kulia ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai.[/caption]

“Kumekuwepo na udanganyifu mkubwa katika usafirishaji wa makinikia kwa makampuni ya madini ya hapa nchini, ambapo yamekuwa yakificha idadi, uzito na thamani ya makinikia yaliyomo katika makontena katika kipindi chote ambacho wamekuwa wakisafirisha madini hayo nje ya nchi,” alifafanua Prof. Osoro.

Aliendelea kwa kusema kuwa mnamo tarehe 27/08/2001 Makontena 48 ya urefu wa futi 20 yenye makinikia yameelezwa kusafirishwa nje ya nchi, hata hivyo iligundulika kupitia hati ya usafirishaji melini Na.Mol-100038 kuwa makontena 67 yenye urefu wa futi 20 ndiyo yaliyosafirishwa hivyo kulikuwepo na makontena 19 zaidi ya idadi iliyooneshwa kwenye hati ya usafirishaji.

Prof. Osoro amesema kuwa jumla ya makontena 44,277 yamesafirishwa nje ya Nchi ikiwa ni kiwango cha chini cha makadirio na kiwango cha juu ni makontena 61,320 kuanzia mwaka 1998 hadi mwezi Machi 2017. Aidha takwimu kutoka katika makampuni yanayosafirisha makinikia yanaonyesha ni makontena 28,000 tu ndio yaliyosafirishwa nje ya nchi kati ya mwaka 1998 nhadi Machi mwaka huu.

[caption id="attachment_3341" align="aligncenter" width="768"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipokea ripoti ya Kamati ya pili ya Uchunguzi wa Madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini sehemu mbalimbali hapa nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa Nehemiah Osoro leo, Ikulu jijini Dar es Salaam. Katikati ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.[/caption] Aidha, Prof. Osoro amesema kuwa kampuni ya Acacia Mining Plc ambayo ilikuwa ikijihusisha na usafirishaji wa makinikia  haitambuliki kisheria kutokana na kutosajiliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) hivyo kufanya biashara hiyo kinyume na sheria.

Aliyataja makampuni ya Bulyanhulu na Pangea Minerals ndio wazalishaji na wasafirishaji wa makinikia nje ya nchi lakini ilibainika kuwa makinikia hayo yalikuwa yakisafirishwa nje ya nchi wakati tayari yameishauzwa.

Prof. Osoro amesema, Kamati imepitia mikataba ya mauzo ya makinikia kati ya makampuni ya uchimbaji na wachenjuaji na kubaini kuwa Serikali siyo sehemu ya mikataba hiyo.

Vile vile mikataba hiyo haina masharti yanayozilazimu kampuni za uchenjuaji kutoa taarifa za uchenjuaji kwa Serikali au muuzaji.

Kamati imetoa mapendekezo kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba Serikali kupitia Msajili wa Makampuni iichukulie hatua za kisheria kampuni ya Acacia Mining Plc ambayo imekuwa ikiendesha shughuli zake nchini kinyume na Sheria.

Vile vile, Serikali iendelee kuzuia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi mpaka hapo makampuni ya madini yanayodaiwa yatakapo lipa kodi, mrahaba na tozo stahiki kwa mujibu wa sheria.

Kamati hiyo pia, imeishauri  Serikali kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya waliokuwa Mawaziri, Wanasheria Wakuu wa Serikali na Manaibu wao, Wakurugenzi wa idara za mikataba, na Makamishna wa madini, wanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini na watumishi wengine wa Serikali ambao wamehusika katika kuingia mikataba ya uchimbaji madini.

[caption id="attachment_3343" align="aligncenter" width="1000"] Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akipokea ripoti ya Kamati ya pili ya Uchunguzi wa Madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini sehemu mbalimbali hapa nchini kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa Nehemiah Osoro leo, Ikulu jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai.[/caption]

Rais Dkt. John Pombe Magufuli, ameipongeza kamati hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya na kusikitishwa namna ambavyo viongozi wachache wamesababisha Tanzania kuwa nchi maskini kwa kusaini mikataba isiyo na maslahi kwa nchi na Watanzania kwa ujumla.

“Wapo watu wanaishi maisha ya ajabu sana, watoto wanakufa kwa kukosa dawa, wakulima wanakosa pembejeo na wapo Watanzania waliokufa kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu. Kumbe wapo viongozi ambao wamekuwa ni sehemu ya kuisababishia nchi umaskini,” alieleza Rais Magufuli.

Aliendelea kwa kusema kuwa mara nyingi Watanzania wamekuwa wakishughulikiwa kwa kutosajiliwa kama vile wamachinga wakati kumbe hata hiyo kampuni ya Acacia Mining Plc haijasajiliwa na haitambuliki kisheria lakini imekuwa ikifanya biashara za mamilioni nchini.

Rais Magufuli amesema kampuni hizo za madini zilieleza zinasafirisha mchanga wenye madini aina tatu tu ambazo ni dhahabu, fedha na shaba lakini kumbe mchanga huo una zaidi ya madini 12.

[caption id="attachment_3345" align="aligncenter" width="1000"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na wasanii pamoja na wajumbe wa Kamati ya Pili ya Uchunguzi wa Madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini sehemu mbalimbali hapa nchini na mara baada ya hafla ya kukabidhiwa ripoti ya Kamati hiyo kumalizika leo Ikulu jijini Dar es Salaam.[/caption]    

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi