Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Haina Kesi za Kodi za Shilingi Trilioni 360
Sep 23, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Habiba Kassim

Serikali imesema kuwa haina kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya Shilingi trilioni 360 na Dola za Marekani milioni 181.4 ambazo hazijaamuliwa katika Bodi ya Rufaa za Kodi (TRAB) na Baraza la Rufaa la Kodi (TRAT) bali kuna mashauri 854 yaliyo kwenye hatua mbalimbali za usikilizaji yenye kodi inayobishaniwa ya jumla ya Shilingi trilioni 4.21 na Dola za Marekani milioni 3.48.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dk. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina, aliyetaka kujua sababu inayofanya kesi 1,097 za kodi za muda mrefu zenye thamani ya Shilingi trilioni 360 na Dola za Marekani milioni 181.4 hazijaamuliwa hadi sasa.

Akifafanua kuhusu kiasi cha Shilingi bilioni 700 kilichopokelewa na Serikali, Mhe. Nchemba alisema kuwa kiasi hicho kilikuwa sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa baada ya kuundwa timu ya kusimamia makubaliano hayo mwaka 2017/2018 kati ya Serikali na Kampuni ya Barick.

‘‘Makubaliano hayo yaliisha Januari 24, 2020 ambapo Tanzania ilikubali kuachilia Shilingi trilioni 360 ili kumaliza shauri lile na kuunda Kampuni ya Twiga ambapo Serikali ina ubia asilimia 16 na Kampuni ya Barick ina asilimia 84’’, alisema Mhe. Nchemba.

Alisema makubaliano hayo pia yaliifanya Kampuni ya Barick kufuta kesi iliyofungua dhidi ya Tanzania iliyokuwa na madai ya Dola za Marekani bilioni 2.7 na kukubaliana Kampuni hiyo itoe Dola za Marekani milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa barabara, pia kutoa Dola za Marekani 6 kwenye kila dhahabu na Dola za Marekani milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya madini.

Aidha, Mhe. Nchemba ameeleza kuwa kwa sasa taasisi za rufaa za kodi zinaendelea kusikiliza mashauri hayo pamoja na mashauri mapya yanayoendelea kusajiliwa kwani idadi ya mashauri ya kodi hupungua au kuongezeka kulingana na kasi ya usikilizaji na usajili kwa nyakati tofauti.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi