Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Aitaka PAPU Kutumia Mashirika ya Ndege ya Afrika
Sep 02, 2023
Rais Samia Aitaka PAPU Kutumia Mashirika ya Ndege ya Afrika
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Dkt. Sifundo Moyo wakati wakivuta kamba kuashiria ufunguzi wa Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU Tower) lililopo eneo la Philips Jijini Arusha tarehe 02 Septemba, 2023.
Na Immaculate Makilika – MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameutaka Umoja wa Posta Afrika (PAPU) kutumia mashirika ya ndege ya Afrika katika usafirishaji wa vifurushi ili kuendelea kuonesha umuhimu wa huduma za posta barani humo.

Amesema hayo leo jijini Arusha wakati akizindua jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika, hafla iliyohudhuriwa na Mawaziri wanaosimamia Sekta ya Posta kutoka katika nchi za Liberia, Afrika Kusini, Uganda, Malawi na Tanzania pamoja na wadau wa posta kutoka nje ya Bara la Afrika.

“PAPU ifanye mashirika ya posta Afrika kusafirisha vifurushi ndani ya Bara la Afrika, sasa posta ilazimishe ndege zetu kusafiri katika nchi za Afrika kupelekea vifurushi. Posta Afrika iwe na maduka ambayo yatawarahisishia wafanyabiashara kufanya shughuli zao”, ameeleza Rais Samia.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Dkt. Sifundo Moyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. Mhe. Nape Nnauye pamoja na viongozi wengine wakati akikata utepe kuashiria ufunguzi wa Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU Tower) lililopo eneo la Philips Jijini Arusha tarehe 02 Septemba, 2023. 

Ameongeza “Sina shaka PAPU inaweza kufanya mageuzi makubwa kuleta mabadiliko ya kidijitali katika utoaji wa huduma za posta ndani ya Afrika ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia pamoja na kutimiza mahitaji ya wateja”.

Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa Afrika inaweza kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa kufanyabiashara ndani ya bara hilo.

“Ni wakati sasa wa Afrika kufanyabiashara kati ya nchi zetu, ndani ya Bara la Afrika. Na Posta Afrika tupo tayari kuwezesha kuongezeka kwa kiwango cha biashara kati ya nchi za bara hili", alisema Waziri Nape.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye, Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Dkt. Sifundo Moyo pamoja na viongozi wengine kwenye picha ya pamoja mara baada ya kufungua Jengo la Makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika (PAPU Tower) lililopo eneo la Philips Jijini Arusha tarehe 02 Septemba, 2023. 

Jengo la PAPU linatajwa kuwa alama muhimu ya umoja na ushirikiano ulipo katika nchi za bara hilo na litasaidia kuboresha utendaji kazi wa shughuli za posta kwa mafanikio zaidi.

Aidha, uzinduzi wa jengo hilo ulitanguliwa na mikutano kadhaa iliyohusisha watunga sera, wasimamizi na waratibu wa sekta ya posta kutoka ndani na nje ya Afrika ambapo walijadili masuala mbalimbali ya kuboresha sekta hiyo ikiwemo matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utoaji wa huduma za posta sambamba na kuchangia uchumi za nchi za kiafrika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi