Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kufanya ubunifu wa kuibua na kupambana na kero za wananchi kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazohusika na kero hizo.
Mhe. Dkt Samia amesema hayo leo Machi 28, 2024 Ikulu jijini Dodoma wakati akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/2023 pamoja na taarifa ya utendaji kazi wa TAKUKURU kwa mwaka 2022/2023 ambapo alisema ubunifu wa TAKUKURU umepunguza kero kwa wananchi.
“Nawapongeza TAKUKURU kwa ubunifu mpya wa uibuaji wa kero kwa kushirikiana na wananchi kwamba wanakwenda chini, wanakaa na wananchi ambapo wananchi wanaeleza kero zao kisha wanazichukua kero hizo na kuzipeleka taasisi husika ambako zinafanyiwa kazi. Utaratibu huu unatusaidia kupunguza kero kwa wananchi na kuifanya serikali iwajibike ipasavyo,” alisema Mhe. Rais Samia.
Akiongelea manufaa ya ripoti zilizowasilishwa alisema ripoti hiyo inaisaidia kupunguza hasara kwani mashirika yanaendelea kupunguza makosa yanayosababisha hasara ili yasijirudie mwaka unaofuata. Faida nyingine ni kuleta uwazi na uwajibikaji kwani wakati ripoti hiyo inapowasilishwa inaweka wazi mchakato wa kuiendesha serikali ikiweka wazi changamoto na mafanikio hivyo kuimarisha uwazi na uwajibikaji.
Alisema ripoti hizo zinazosomwa kila mwaka zinachangia maboresho na kuimarisha utendaji kazi ndani ya serikali kwani dosari zilizobainishwa mwaka husika zinafanyiwa kazi ili kutoendelea kujitokeza miaka ya usoni na kwamba kwa utaratibu huo utafika wakati hakutakuwa na hasara katika uendeshaji wa mashirika.
“Tumesikia ongezeko la hati safi kwa sababu CAG anatoa ripoti yake na watendaji wanaposikia wanakwenda kurekebisha matokeo yake tuna asilimia 99 (99%) ya hati safi. Ripoti hizi zinatusaidia pia kwenye kuongeza ukusanyaji wa mapato kutokana na vipengele mbalimbali anavyovionyesha CAG na TAKUKURU mapato yanarudi serikalini,” alihitimisha Mhe. Dkt. Samia.