Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Nyama Yaongoza Mauzo ya Nje, Sekta ya Mifugo
Sep 06, 2023
Nyama Yaongoza Mauzo ya Nje, Sekta ya  Mifugo
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega akizungumza ikiwa na sehemu ya Mkutano kuelekea Kilele cha Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaoendelea kufanyika Jijini Dar es Salaam
Na Georgina Misama – MAELEZO

Serikali imesema Sekta ya Mifugo ni shughuli kubwa ya kiuchumi katika kaya zisizopungua milioni 2.2 za Tanzania sawa na asilimia 35 ya kaya zote ikichangia uzalishaji wa tani 805,000 za nyama, lita bilioni 3.6 za maziwa, mayai bilioni 5.5, vipande vya ngozi na ngozi milioni 14.1 kwa mwaka 2023.

Akiongea leo katika mdahalo maalum uliohusu masuala ya sekta hiyo ikiwa na sehemu ya Mkutano kuelekea Kilele cha Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF) unaofanyika Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema mazao ya mifugo yanachangia ulaji wa nyama kg 15, lita za maziwa 62 na mayai 106 kwa mwaka dhidi ya viwango vinavyopendekezwa vya  nyama kg 50,  maziwa lita 200 na mayai 300.

“Thamani ya mauzo ya nje kwa upande wa Sekta ya Mifugo ni tani elfu 14.7 za nyama, lita 65,000 za maziwa na vipande 800,000 vya ngozi ambapo kwa pamoja zinaingiza milioni 61.4 kwa mauzo ya nyama, 435 elfu kwenye mauzo ya maziwa na Dola za Kimarekani milioni 2.4 kwenye mauzo ya ngozi na kwamba Sekta ya mifugo imejaaliwa kuwa na fursa mbalimbali zinazofaa kwa uwekezaji,”alisema Mhe. Ulega.

Amesema Tanzania ina idadi kubwa ya rasilimali za mifugo takribani milioni 77 na kwamba ni shughuli kubwa ya kiuchumi katika kaya milioni 2. 2 na kwamba inachangia uzalishaji wa kila mwaka wa tani 805,000 za nyama, lita bilioni 3.6 za maziwa, mayai bilioni 5.5, vipande milioni 14.1 vya ngozi.

“Tumeimarisha Sekta hii kwa kuboresha mifugo kwa njia ya upandishaji mbegu na matumizi ya ng'ombe bora wa kuzaliana, kuboresha uendelezaji wa malisho na maji kwa kuanzisha mashamba ya biashara kwa ajili ya uzalishaji wa mbegu za malisho na malisho, kuimarisha mifumo ya afya ya wanyama kupitia kampeni za chanjo na udhibiti wa kupe na magonjwa yanayoenezwa na kupe,” amesema Mhe. Ulega.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi