Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Nelson Mandela Yapongezwa Muundo Mzuri wa Utoaji Elimu
Mar 05, 2024
Nelson Mandela Yapongezwa Muundo Mzuri wa Utoaji Elimu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa (katikati) akipata maelezo kuhusu matumizi ya Kituo cha Kufundia Kidigitali (C-CODE) kutoka kwa Mtaalamu wa Tehama, Bw. Octavuani Kanyengele (kushoto) na kulia ni Makamu Mkuu wa Taasisi, Prof. Maulilio Kipanyula wakati wa ziara ya kikazi katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Machi 5,2024.
Na Lorietha Lawrence

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhamed Mussa ameipongeza Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha kwa muundo mzuri wa utoaji wa elimu ambao unazalisha wataalamu wenye weledi unaowezesha wahitimu kuweza kujiajiri mara baada ya kuhitimu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa (kulia) akipata maelekezo kutoka kwa Makamu wa Taasisi, Prof. Maulilio Kipanyula wakati wa ziara ya kimkakati katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Machi 05, 2024.

Mhe. Lela amesema hayo machi 5, 2024 alipotembelea Taasisi hiyo kwa lengo la kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa ikiwa ni kuona namna ya taasisi na vyuo vya elimu ya juu nchini Tanzania vinavyojiendesha.

 

“Naupongeza uongozi wa Taasisi kwa uwekezaji mkubwa mlioufanya na kitu kikubwa nilichojifunza katika taasisi hii ni kujikita katika kufanya tafiti, na sisi tumekuja kujifunza ili kuleta magaeuzi kupitia chuo Kikuu cha Zanzibar (Suz) ili kuangazia taasisi zetu ambazo tunaweza kuzikita katika masuala ya tafiti ili kutatua changamoto mbalimbali za jamii”, amesema Mhe.Lela

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa akipata maelezo kuhusu bunifu zinazofanywa na wabunifu kutoka Kituo cha Tehama wakati wa ziara ya kimkakati katika Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Machi 05, 2024.

Ameongeza kuwa, taasisi hiyo imefanya vyema kwa kuanzisha Ndaki ya Biashara na Jamii ili kuwezesha wataalam wa bunifu na tafiti mbalimbali kuwa na akili ya biashara pale wanapohitimu elimu yao.

 

Aidha, ametoa wito kwa taasisi za elimu ya juu kujifunza kutoka katika taasisi ya Nelson Mandela ili kuwajengea uwezo na kuwawezesha wahitimu kibiashara na kidijitali kwa manufaa binafsi na jamii kwa ujumla. 

 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Muhammed Mussa (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, alipofanya ziara ya kimkakati katika Taasisi hiyo Machi 05, 2024.

Naye Makamu Mkuu wa Taasisi, Prof. Maulilio Kipanyula ameahidi kuendeleza ushirikiano na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar ili kukuza elimu katika fani mbalimbali ikiwemo tafiti, bunifu, sayansi na Teknolojia.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa TEHAMA Idara ya Elimu Zanzibar, Bw. Mbwana Yahya Mwinyi ameeleza kufurahishwa na mipangilio ya TEHAMA katika taasisi, hivyo kuangalia namna ya kushirikiana kwa karibu katika kukuza na kuendeleza sekta ya elimu nchini.

 

Katika ziara yake Mhe. Lela amefanikiwa kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Kituo cha Kisasa cha Elimu Kidigitali C-CODE), ICT Resource center na kituo Atamizi kwa ajili ya kuatamia bunifu za wanataaluma ambapo ni maeneo muhimu katika Taasisi yanayotumika kukuza bunifu za wataalamu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi