Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kwa kushirikiana na Umoja wa Posta Afrika (PAPU) wamesaini hati ya makubaliano kwa ajili ya kushirikiana zaidi katika masuala ya kidijitali, katika bunifu zitakazochagiza utendaji kwenye sekta ya posta kwa kutumia mifumo ya kidijitali lengo ikiwa ni kuendana na wakati pamoja na mahitaji ya soko.
Uwekaji wa saini ya hati ya makubaliano hayo umefanyika jijini Arusha, Machi 7, 2024 ambapo Makamu Mkuu wa Taasisi ya Nelson Mandela (NM-AIST), Prof. Maulilio Kipanyula alisema ushirikiano huo utawezesha kutoa matokeo ya utafiti wa kidijitali .
Alisema endapo tafiti zinazofanyika kwenye taasisi hiyo zikiunganishwa na huduma za Posta zitaimarisha tafiti na bunifu katika masuala ya teknolojia zitakazosaidia uendeshaji wa huduma za Posta katika nchi 45.
"Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, biashara nyingi zinafanyika kwa njia ya mtandao kupitia E-commerce hivyo biashara hii ikiungana na tafiti itawezesha uchumi kukua kwa kiasi kikubwa", alisema Prof. Maulilio Kipanyula.
Alisisitiza kuwa, Nelson Mandela ina Shule Kuu ya Hisabati, Sayansi na Uhandisi wa Ukokotoaji na Mawasiliano (CoCSE) kwa ajili ya masuala ya TEHAMA pia ina wataalam wabobezi katika matumizi ya akili bandia, matumizi ya data sayansi ikiwemo kituo maalum cha TEHAMA cha kuchakata takwimu nyingi kwa wakati mmoja zinazosaidia ukuzaji uchumi na teknolojia katika sekta ya tafiti.
Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU), Dkt. Sifundo Chief Moyo alisema ushirikiano walioingia kati ya PAPU na NM-AIST ni kielelezo tosha katika masuala ya bunifu na tafiti zaidi katika masuala ya teknolojia katika utoaji wa huduma za posta kwa nchi za Afrika.
Alisema ili sekta ya posta iweze kukua lazima iweze kupata mbinu za kukuza masuala ya tafiti katika masuala ya sayansi na teknolojia katika kuhakikisha biashara zinazotolewa zinakuza uchumi zaidi katika nchi za Afrika pamoja na kuleta mwamko zaidi kwa watumiaji huduma hizo kwenye ubora wa biashara na ukuzaji uchumi.