Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Nchi Haiwezi Kufanikiwa kama Hatutalipa Kodi - Msigwa
Mar 12, 2025
Nchi Haiwezi Kufanikiwa kama Hatutalipa Kodi - Msigwa
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 12, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa amewasisitiza Watanzania kuendelea kulipa kodi inavyotakiwa ili nchi iweze kutimiza maono na mipango iliyojipangia.

Bw. Msigwa ametoa rai hiyo leo Machi 12, 2025 jijini Dodoma  katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO wakati wa mkutano wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda na Waandishi wa Habari kuelezea utekelezaji wa mamlaka hiyo ndani ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Ameeleza kuwa, ni vizuri kila Mtanzania kujua kuwa akilipa kodi amejijenga yeye mwenyewe na asidhani kwamba akilipa kodi inaliwa na mtu mwingine kwani kodi inarudi kuwahudumia Watanzania wenyewe.

"Nawapongeza TRA kwa kupiga hatua kubwa katika ukusanyaji wa kodi, tutapanga mipango na maono mengi sana mfano sasa hivi tunatengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 lakini ukweli ulio wazi, haya yote hayawezi kufanikiwa kama hatulipi kodi", amesema Bw. Msigwa.

Amefafanua kuwa, kipimo cha kwanza cha kuangalia biashara ya mtu inaenda vizuri ni pale anapolipa kodi inavyotakiwa, hivyo ametoa rai kwa Watanzania kusikia fahari kulipa kodi kwani kukwepa kodi sio ujanja.

Akielezea kuhusu programu hiyo inayoratibiwa na Idara ya Habari na Taasisi za Umma kuelezea utekelezaji wa taasisi zao ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Bw. Msigwa amesema kuwa tangu Februari 17, 2025 mpaka leo, jumla ya Taasisi za Umma 17 zimeshazungumza na Watanzania.

 

"Ratiba hii itaendelea mpaka Machi 27, 2025 na baada ya hapo, Aprili 14, 2025 tutaanza na Waheshimiwa Mawaziri nao watakuja kuzungumza na Watanzania kuhusu utekelezaji wa wizara zao ndani ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita", amesema Bw. Msigwa.

Aidha, ameeleza kuwa taasisi nyingi zimeonesha utayari wa kuja kuzungumza na Watanzania, hivyo wizara imekubali kutoa nafasi nyingine kwa taasisi kuendelea kuwaeleza Watanzania kazi zilizotekelezwa ndani ya miaka minne.

Katika hatua nyingine, amewapongeza Waandishi wa Habari kwa namna wanavyotangaza na kuwahabarisha  Watanzania yale yanayoelezwa na taasisi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi