Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

NCAA, JKT Wasaini Mkataba Ujenzi Nyumba 5000
Sep 26, 2023
NCAA, JKT Wasaini Mkataba Ujenzi Nyumba 5000
Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dkt. Freddy Manongi (kulia) akipeana mkono mara baada ya kusaini mkataba wa Makubaliano na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia SUMA- JKT kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba 5,000 za wananchi wanaoishi katika Hifadhi ya Ngorongoro
Na Kassim Nyaki - Arusha

Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi  ya Ngorongoro (NCAA) imesaini mkataba wa Makubaliano na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia SUMA- JKT kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba 5,000 za wananchi wanaoishi katika Hifadhi ya Ngorongoro ambao wanaendelea kujiandikisha kwa ajili ya kuhama kwa hiari.

Kwa mujibu wa Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dkt. Freddy Manongi amesema kuwa, Mradi wa ujenzi wa nyumba hizo 5,000 unatarajiwa kuanza mwezi Oktoba, 2023 na tayari Serikali imeshatenga shilingi bilioni 97  ambapo mradi huo unatarajia kukamilika katika kipindi cha miezi sita ijayo.

Katika awamu ya kwanza  ya utekelezaji wa zoezi hilo nyumba zaidi ya 500 zilijengwa na tangu zoezi hilo lilipoanza mwezi Juni, 2022, tayari makundi 19 yenye kaya zaidi ya 565 watu 3,097 na mifugo zaidi ya 15,500 imeshahama ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Hamasa ya wananchi kujiandikisha kuhama kwa hiari imeendelea kuongezeka ambapo hadi sasa jumla ya Kaya 1524  zimeshajiandikisha kuhama kwa hiari.

Kamishna Dkt. Manongi ameeleza kuwa katika utekelezaji wa awamu inayofuata pamoja na wananchi kuhamishiwa nyumba zinazojengwa na Serikali lakini wananchi watapewa uhuru wa kuhamia mahali popote wanapotaka na Serikali itawapa stahiki zao kwa mujibu wa sheria.

Serikali itaendelea kuhamisha wakazi wa Ngorongoro walioomba kuhama kwa hiari kwa kuzingatia misingi ya haki za kibinadamu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi