Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Ulega Ahimiza Ufugaji Ng'ombe wa Maziwa
Oct 27, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM IRINGA

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewahimiza wananchi wa Mufindi mkoani Iringa kuhakikisha wanafuga ng’ombe wa maziwa kwa ajili ya kujipatia kipato.

Ulega alisema hayo Oktoba 26, 2022 wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika vijiji 975 ilipofanya ziara katika kijiji cha Kibengu wilayani Mufindi mkoa wa Iringa.

Akitolea mfano wa uwepo kiwanda cha maziwa cha Asas mkoani Iringa kuwa, ni moja ya fursa kwa wananchi wa wilaya hiyo kuanza mchakato wa kuwa na ng’ombe wa maziwa kwa sababu upo uhitaji mkubwa wa maziwa hasa kipindi hiki ambacho kiwanda cha Asas kinaongezwa sambamba na kuwa na mpango wa kutengeneza maziwa ya unga.

"Iringa ni wakulima wazuri wa mahindi na miti, nashauri kila nyumba katika maeneo yake kuwa na ng’ombe wawili au watatu wa maziwa", alisema Ulega.

Aliongeza kwa kusema kuwa, ni vyema wananchi wa Mufindi na wilaya nyingine za mkoa huo wanapomaliza kutumia mahindi basi wawe na maziwa ambayo sehemu yanaweza kutumiwa na watoto na kiasi kingine kikatumika kwa ajili ya biashara.  Alisema, katika jitihada ambayo Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaenda kufanya ni kuimarisha shamba lake la Sao Hill la Mitamba lilipo Iringa kwa lengo la kuboresha sekta ya mifugo.

Alisema, mbali na juhudi mbalimbali zinazofanywa katika kuboresha sekta ya mifugo, moja ya jambo wizara yake itafanya ni kuzungumza na uongozi wa mkoa huo kwa kushirikiana na  kiwanda cha maziwa cha Asasi  na Benki ya Kilimo pamoja na Shirika la PASS ni kuanzisha mradi ambao wale wananchi walio tayari basi waweze kukopeshwa ng’ombe wa maziwa ili wakati analima mahindi basi wawe pia na ng’ombe wa maziwa na baadaye kuwa na vituo vya kukusanya maziwa,  jambo litakalowapa uhakika wa kila siku kupata takriban Shilingi 10,000.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi