Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Kihenzile Aitaka TAA Kuvunja Mkataba Kiwanja cha Ndege Songea
Feb 24, 2024
Naibu Waziri Kihenzile Aitaka TAA Kuvunja Mkataba Kiwanja cha Ndege Songea
Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Songea, Mhandisi Danstan Komba (kushoto) wakati alipokagua Kiwanja cha Ndege cha Songea mkoani Ruvuma mwishoni mwa wiki.
Na Administrator

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameitaka Mamlaka ya Viwanja  vya Ndege Tanzania (TAA) kuvunja mkataba na Mkandarasi Kampuni ya Manyanya Enginnering Company Limited kutokana na Mkandarasi huyo kushindwa kukamilisha mradi wa jengo la abiria kwa wakati.

 

Naibu Waziri Kihenzile ametoa maagizo hayo mkoani Ruvuma mara baada ya kukagua mradi huo na kutoridhishwa na maendeleo ya utakelezaji wake ambao ulitakiwa kuwa umekamilika mwishoni mwa mwaka 2023. 

 

“Serikali imewekeza takribani bilioni 37 ili kuboresha miundombinu mbalimbali katika kiwanja hiki, na mkandarasi wa Jengo la abiria amelipwa muda mrefu fedha za kuanza mradi huu lakini amefanya kazi chache na kutelekeza mradi, hatuwezi kukubaliana na jambo hili ninawaelekeza TAA kuhakikisha mnapitia vipengele vyote vya mradi huu na mvunje mkataba huu maana ameshindwa kukamilisha kwa wakati”, amesema Naibu Waziri Kihenzile. 

Muonekano wa jengo la kuongozea ndege ambalo limekamilika na kuanza kutumika lililopo katika Kiwanja cha Ndege cha Songea. Jengo hilo ni sehemu ya mradi wa maboresho ya miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Songea mkoani Ruvuma.

Naibu Waziri Kihenzile imeitaka TAA kuhakikisha viwanja vya ndege vyote nchini vinapata hati za umiliki ili kupunguza changamoto za uvamizi ambazo zimekuwa zikifanywa na wananchi wanaoishi pembezoni mwa viwanja hivyo.

 

Aidha Naibu Waziri Kihenzile ameipongeza TAA kwa kuendelea kuhakikisha utoaji wa huduma katika viwanja vya ndege nchini unaboreshwa ili kupelekea ongezeko la abiria, mizigo na mashirika ya ndege yanayotoa huduma katika viwanja nchini.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile ameishukuru Serikali kwa kufanya maboresho katika kiwanja hicho kwani yamechochea kukua kwa uchumi wa mkoa huo sababu kukamilika kwake kumekuwa na ongezeko la usafirishaji wa mizigo hususani ya mboga mboga na matunda yanayozalishwa mkoani hapo. 

Muonekano wa barabara ya kuruka na kutua ndege pamoja na taa katika Kiwanja cha Ndege cha Songea. Kukamilika kwa mradi huo ambao ni sehemu ya mradi wa maboresho ya miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Songea kumekiwezesha kiwanja hicho kuweza kutoa huduma kwa saa 24.

Naye Meneja wa Kiwanja hicho, Mhandisi Danstan Komba amesema kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege (Run way), taa za kuongozea ndege, uzio, maegesho ya ndege, barabara ya kiungio (Taxing Way) na kituo cha nishati kumekifanya kiwanja hicho kuongeza wigo wa utoaji wa huduma ikiwemo kutumika kwa saa ishirini na nne (24).

Muonekano wa sehemu ya maegesho ya ndege iliyokamilika katika Kiwanja cha Ndege cha Songea. Mradi huo ni sehemu ya mradi wa maboresho ya miundombinu ya Kiwanja cha Ndege cha Songea mkoani Ruvuma.

Mhandisi Komba amemuhakikishia Naibu Waziri Kihenzile kuwa TAA itachukua hatua stahiki dhidi ya Mkandarasi huyo ili kuhakikisha mradi wa jengo la abiria unakamilika na kurahisisha utoaji wa huduma za abiria wanaotumia kiwanja hicho.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi