Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Chillo Ataka Elimu ya Kusimamia Sheria za Utunzaji Mazingira
Oct 18, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM Simiyu

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Mhe. Khamis Hamza Chilo amewataka viongozi wa mikoa na wilaya nchini kwenda kuwafundisha wananchi namna bora ya kusimamia sheria na taratibu za utunzaji na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Pia ametaka viongozi hao kuelimisha namna ya kufuata na kutekeleza sheria zitakazolinda mazingira, ardhi na  maliasili wakiwemo wanyama pori na mapori ya akiba.

Chillo alitoa kauli hiyo Oktoba 17, 2022 kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na wananchi wa kata ya Ihusi-Bariadi, mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara wakati kamati ya Mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya ardhi ya Vijiji 975.

Alisema, miongoni mwa vitu vikubwa ambavyo Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta imebaini wakati wa ziara zake ni upungufu na uchache wa usimamizi wa sheria hasa zile sheria za mazingira.

Kwa mujibu wa Chillo, moja ya njia sahihi ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi bila kuleta taharuki kama ilivyoelekezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ni kwenda kuwafundisha wananchi kipi kipo kwenye sheria .

‘’Twendeni kufundisha namna bora ya kusimamia sheria na taratibu za utunzaji na uhifadhi vyanzo vya maji, ni masafa gani wananchi wanatakiwa kufuga ama kujenga kutoka chanzo cha maji maana kinyume na hapo kila siku tutakuwa tunalia mazingira, maliasili, ardhi pamoja na migogoro’’. Alisema Chillo

Naibu Waziri huyo Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulia Mazingira alibainisha kwa kusema kuwa, bila kutoa elimu ya namna ya kusimamia sheria na taratibu za utunzaji na uhifadhi mazingira, Serikali itaingia mzigo mkubwa wa kuzunguka, kusema na kueleza tu kwa sababu tu kuna mambo hayajasemwa mwanzo.

‘’Tukawaambie watu wetu watunze vyanzo vya maji kinyume na hapo hatutakuwa na maliasili, hatutakuwa na rasilimali kwa sababu vyanzo vya maji ni fahari yetu watanzania.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Chilo, mpaka kesho bado wapo watu wanalima kwenye  vyanzo vya maji, lakini wapo pia wengine wanapelekea mifugo kwenye vyanzo hivyo huku wengine wakiendesha shughuli za uchimbaji madini ambapo matokeo yake ni kuharibu vyanzo vya maji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi