Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Msizifanyie ‘’Lamination’’ Hati MilIki za Ardhi - Mhandisi Sanga
Mar 19, 2024
Msizifanyie ‘’Lamination’’ Hati MilIki za Ardhi - Mhandisi Sanga
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga (Kulia) akisalimiana na wenyeji wake mara baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii mkoani humo.
Na Munir Shemweta, CHALINZE

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga amesema hati miliki za ardhi zinazotolewa kwa wamiliki wa ardhi nchini haziruhusiwi kuwekewa ‘’Lamination’’.

Mhandisi Sanga ametoa kauli hiyo tarehe 18 Machi 2024 wilayani Chalinze mkoani Pwani wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Ardhi, Maliasili na Utalii kukagua utekelezaji Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo la Msolwa.

“Hati unayopewa mwananchi hautakiwi kuifanyia lamination, kwanza ijulikane zipo hati za zamani zilizowekewa kitabu kama majalada na zile mpya” alisema Mhandisi Sanga.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, mmiliki wa ardhi anaweza kutaka kuuza ardhi ama nyumba yake kwa mtu mwingine ama kutaka kuchukulia mkopo, hivyo hati yake inabidi igongwe muhuri na kama ikifanyiwa ‘’lamination’’ itakuwa ngumu kugongwa muhuri.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga (kulia) akisalimiana na Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakati wa ziara ya Kamati hiyo mkoani Pwani.

Kwa mantiki hiyo, Mhandisi Sanga ameweka wazi kuwa, ndiyo maana wizara yake ya ardhi inashauri hati miliki za ardhi zisifanyiwe ‘’lamination’’ ili mmiliki anapotaka kufanya muamala wowote basi hati yake iweze kufanyiwa.

“Lakini hata zile hati miliki mpya za kieletroniki hali kadhalika, maana hata hizo zina ‘electronic feature’ mle ndani yaani kuna vitu vinavyofanya iwe hati ya  kipekee lakini pia ina bacon, mambo ya kisasa kidogo hiyyo ukifanya ‘’lamination’’ mambo yote hayo huwezi kuyafanya”, alisema Mhandisi Sanga.

Amebainisha kuwa, wizara yake ya ardhi itaendelea kutoa elimu juu ya suala hilo sambamba na kutoa maagizo kwa watendaji wote wa sekta ya ardhi kuweka matangazo kwenye ofisi zao kuhakikisha wananchi wanapata elimu kwamba hati miliki ya ardhi haitakiwi kufanyiwa ‘’lamination’’ iwe mpya au ya zamani ili kumsaidia mwananchi mwenye hati kufanya muamala anaotaka kufanya.

Kamati ya Kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii imehitimisha kutembelea na kukagua miradi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi tarehe 18 Machi, 2024 ambapo katika ziara zake imeweza kukagua mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP) katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Mkoa wa Lindi, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni Dar es Salaam pamoja na mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi katika eneo la Msolwa lililopo Halmashauri ya Chalinze Mkoa wa Pwani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi