Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mpango wa Kuimarisha Huduma ya Maji Buswelu Waanza
Sep 02, 2023
Mpango wa Kuimarisha Huduma ya Maji Buswelu Waanza
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), Neli Msuya akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mitaa ya Kigala, Busenga, Bulola A , Bujingwa na Buhila baada ya zoezi la kukabidhi matenki kwa viongozi hao kukamilika
Na Mwandishi Wetu - MWAUWASA

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) imetekeleza mpango wa muda mfupi wa kupunguza changamoto ya majisafi katika Kata ya Buswelu.

Mpango huo umehusisha kazi ya kukabidhi matenki ya maji yenye uwezo wa kuhifadhi lita 45,000 ambayo yatasambazwa katika maeneo yenye changamoto ndani ya Kata ya Buswelu.

Akizungumza wakati wa kikao kifupi kilichoenda sambamba na zoezi la kukabidhi matenki kwa Viongozi wa Mitaa ya Kigala, Busenga, Bulola A , Bujingwa na Buhila, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Neli Msuya amesema kuwa MWAUWASA imefikisha matenki hayo kwenye Kata ya Buswelu ikiwa ni suluhisho la muda mfupi la upatikanaji wa maji wakati Mamlaka ikiwa inafanya jitihada za muda mrefu za kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji inapatiwa ufumbuzi.

"Hatua hii ni suluhisho la muda mfupi katika kuhakikisha angalau changamoto ya ukosefu wa maji inapungua katika Kata ya Buswelu, tunaendelea na utekelezaji wa mradi wa maji Butimba ambao utaongeza kiasi kikubwa cha maji katika maeneo ya Kata ya Buswelu," amesema Neli.

Amesema MWAUWASA inashirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria kufanya utafiti wa maji yaliyopo ardhini pamoja na kufufua visima vilivyoacha kutumika kwa sababu mbalimbali.

"Lengo letu ni kuhakikisha tunatumia kila rasilimali zilizo ndani ya uwezo wetu kumaliza changamoto ambayo inatukabili, kwa msaada wa wataalam wa RUWASA pamoja na Bonde ya Ziwa Victoria tutapita katika visima vilivyoacha kutumika ili tuangalie uwezekano wa kusambaza maji hayo kwa wananchi na kupunguza changamoto," ameeleza Ndugu Neli.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Buswelu, Sarah Ng'wani ameishukuru MWAUWASA kwa kutekeleza mpango huo wa muda mfupi na kutoa rai kwa MWAUWASA kuja na mipango mingine ili kuondoa changamoto ya maji kwa Buswelu.

"MWAUWASA imetupa  matumaini ya kutatua changamoto ya maji kwenye Kata yetu. Niwaombe kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi, sisi tuko tayari kutoa ushirikiano pale tutakapohitajika." Alimalizia Bi. Sarah.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi