Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mkutano wa Wadau Kujadili Mapitio ya Sera ya Elimu na Mitaala Kufanyika kwa Siku Tatu Jijini Dodoma - Waziri Mkenda
Sep 25, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mathias Canal, WEST-Dodoma

Serikali imeandaa mkutano maalumu kwa mara nyingine wa wadau wa elimu kutoka maeneo na sekta mbalimbali nchini kote nchini.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma leo tarehe 25 Septemba, 2022 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof . Adolf Mkenda amesema kuwa mkutano huo unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 26 hadi 28 Septemba 2022 Jijini Dodoma.

Waziri Mkenda ameeleza lengo la Mkutano huo kuwa ni kujadili Mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na Mabadiliko ya Mitaa ya Elimu msingi. 

Amesema kuwa majadiliano hayo yatatokana na hatua iliyofikiwa na mapitio hayo kupitia kamati maalumu zilizopewa majukumu hayo.

Waziri Mkenda amesema kuwa mkutano huo unajumuisha Wahadhiri, Waajiri, Wadau wa Maendeleo, Taasisi za umma na Binafsi, Taasisi za Dini, Taasisi zinahusika na uendelezaji wa lugha, Wabunge, Wajumbe toka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Taasisi zisizo za Kiserikali, Jumuiya za kitaaluma na Taasisi za Sayansi na Utafiti.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mkenda amesema kuwa tarehe 27 Septemba, 2022, Serikali itatangaza rasmi majina ya wanafunzi waliofaulu kwa kiwango kikubwa katika masomo ya Sayansi ambao watastahili kupata ufadhili wa SAMIA SCHOLARSHIPS endapo watadahiliwa kusoma masomo ya Sayansi, Elimu tiba na Uhandisi kwenye vyuo mbalimbali ndani ya nchi.

"Mtakumbuka Wizara yetu ilitoa ahadi kupitia hotuba ya bajeti ya kuanzisha programu mpya ya kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa wahitimu bora wa kidato cha sita katika masomo ya Sayansi ambapo mpaka sasa tuna majina karibu 600 ya wanafunzi ambao wamepata ufaulu wa kiwango kikubwa katika masomo hayo" Amekaririwa Waziri Mkenda

Kadhalika, Waziri Mkenda ameukumbusha umma kuwa Serikali imezindua tuzo za waandishi bunifu zijulikanazo kama Tuzo za Mwalimu Nyerere, hivyo ameendelea kukaribisha Waandishi Bunifu wa Riwaya na Mashairi kuwasilisha maandiko yao ili kuwania tuzo hizo. 

Prof. Mkenda amesema kuwa Mwisho wa kupokea Mawasilisho hayo ni  Novemba 30, 2022 ambapo kwa taarifa zaidi kuhusu tuzo hizo na maulizo wanaweza kufuatilia katika akaunti maalumu za mitandao ya kijamii za  tuzo Nyerere au mitandao na tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Taasisi ya Elimu Tanzania-TET kwa anuani ya tuzonyerere@tie.go.tz

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi