[caption id="attachment_3335" align="aligncenter" width="630"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akipitia ripoti ya Kamati ya pili ya Uchunguzi wa Madini yaliyo kwenye makontena yenye mchanga unaosafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini sehemu mbalimbali hapa nchini mara baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo leo, Ikulu jijini Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.[/caption]
Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameigiza Wizara ya Katiba na Sheria kuunda timu ya wataalam wa sheria kupitia upya sheria za mikataba ya madini nchini na kuzipeleka Bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.
Rais Dkt. Magufuli ametoa maagizo hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam mara baada ya kupokea ripoti na kukubali mapendekezo yote yaliyotolewa na Kamati ya Pili ya kuchunguza mchanga wenye madini (Makinikia).
“Timu ya wataalam wa sheria waaminifu wapitie sheria na mikataba yote ya madini na ipelekwe bungeni hata kama itahitajika kuongeza muda wa bunge”. Aliagiza Dkt. Magufuli.
Moja ya mapendekezo ya Kamati hiyo ni lile linaloitaka Serikali ipitie na kufanya marekebisho au kufuta na kubadili kabisa sheria ya madini na sheria za kodi ili kuondoa pamoja na mambo mengine, masharti yote yasiyokuwa na manufaa kwa taifa ikiwa pamoja na masharti yaliyomo kwenye kifungu thabiti (stability clause) ambacho kinazuia marekebisho ya sera na sheria kuathiri masharti yaliyomo katika mikataba ya uchimbaji madini.
Sambamba na agizo hilo, Rais ameaviagiza pia vyombo vya dola kufanya uchunguzi dhidi ya wote waliohusika na kuingia mikataba mibovu ya madini popote pale walipo na ikithibitika walishiriki kuingia mikataba mibovu ya madini basi hatua za kisheria zichukuliwe mara moja dhidi yao.
Aidha Rais Dkt. Magufuli amewaomba Watanzania kuungana katika kupigana vita ya kuikomboa nchi kiuchumi bila kujali itikadi na dini zao ili Taifa lifaidike na rasilimali zilizopo.
Rais pia amesikitishwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipingana na juhudi za serikali katika kupigania rasilimali kwa kupiga propaganda kuwa nchi itashitakiwa badala ya kuonesha uzalendo wao kwa kutumia utaalam wao wa sheria kuisaidia nchi.
“Tushikamane katika hii vita, hii ni vita ya kiuchumi na ni mbaya maana wasaliti pia wapo. Hivi ni nani anayeweza kuisoma hii ripoti na kufurahia?”. Alihoji Rais huku akiwaomba wanasheria kusimama kidete katika kuisaidia nchi kuondokana na mikataba mibovu ya madini.
Katika hatua nyingine Rais pia ameagiza mikataba mingine kama ile ya gesi nayo ipitiwe upya ili kujiridhisha kama nchi inafaidika na mikataba hiyo.
Nae Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Paramagamba Kabudi amesema kuwa agizo la Rais linaanza kutekelezwa mara moja kwa kupitia mikataba yote ya madini na kuipeleka katika bunge linaloendelea.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mhe. Job Ndugai ameelezea namna Bunge lilivyosikitishwa na taarifa za Kamati zote mbili ambazo zimeonesha jinsi nchi inavyo poteza mapato kutokana na udanganyifu unaofanywa na kampuni za madini.
“Bunge litazitendea haki sheria zote zitakazoletwa kwa ajili ya marekebisho. Na kabla bunge hili halijaisha nitakuwa nimeunda timu ya kufuatilia suala la almasi na baadae madini ya Tanzanite”. Alieleza Spika Ndugai.
Akisoma ripoti hiyo mbele ya Rais, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Profesa Nehemiah Osoro alimtoa hofu Rais, juu ya kupitia upya mikataba hiyo kwa kusema kuwa pamoja na uwepo wa vifungu thabiti, Serikali haizuiliwi kurekebisha au kubadili Sera na Sheria zinazoweza kuathiri mikataba.
Alisema, mkataba wowote ule kisheria, hauwezi kuwa juu ya Mamlaka asili ya nchi (state soveregnity) na maslahi ya umma kuhusu rasilimali zake za asili.
“Mikataba hiyo ina vifungu vinavyoruhusu Serikali na makampuni ya uchimbaji kujadili na kurekebisha sharti lolote la kimikataba. Hivyo, mikataba ya uchimbaji madini inaweza kurekebishwa”. Alieleza Profesa Osoro.
Alisema kuwa kila nchi inasimamia kanuni ya umiliki wa milele wa mali asili zake kwa mujibu wa azimio Na. 1803 la mwaka 1962 la Baraza kuu la Umoja wa mataifa, Azimio Na. 3281 la 1974 la Baraza kuu la Umoja wa Mataifa la Haki na Majukumu ya Kiuchumi ya Mataifa. Maazimio yote yanatamka bila shaka haki na mamlaka ya nchi kuweka mifumo ya kuondoa unyonyaji katika mali asili na kuamua migogoro juu ya
mali asili.
Aprili 10 mwaka huu, Rais aliteua Kamati ya pili ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na makanikia yanasafirishwa nje ya nchi yakiwemo makontena 277 yaliyozuiliwa na serikali katika bandari ya Dar es Salaam.
Kamati hiyo iliongozwa na Mwenyekiti Profesa Nehemiah Osoro na wajumbe saba ambao ni Profesa Longinus Rutasitara, Dr. Oswald Mashindano, Bw. Gabriel Malata, Bw. Casmir Sumba, Bi. Butamo Kasuka, Bw. Bernard Asubisye na Bw. Andrew Massawe.