Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Migogoro Wakulima, Wafugaji Lindi Mkono wa Dola Kuwashukia
Sep 01, 2023
Migogoro Wakulima, Wafugaji Lindi Mkono wa Dola Kuwashukia
Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Mhe. Jumanne Sagini akizungumza na wananchi wakati wa ziara yake katika Wilaya ya Nachingwea, Ruangwa na Wilaya ya Lindi Jimbo la Mchinga mkoani Lindi kutokana na kuwepo kwa migogoro ya Wakulima na Wafugaji ambayo imepelekea mauaji na baadhi ya Mifugo kufa na kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga.
Na Hyasinta Kissima

Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Mhe. Jumanne Sagini amesema Serikali kupitia Jeshi la Polisi haitakuwa na uvumilivu juu ya Mwananchi yeyote awaye Mkulima au Mfugaji ambaye analengo la kuvuruga  Amani na Usalama wa Raia na mali zao.

Naibu Waziri Sagini ameyasema hayo kwenye ziara yake katika Wilaya ya Nachingwea, Ruangwa na Wilaya ya Lindi jimbo la Mchinga Mkoani Lindi kutokana na kuwepo kwa migogoro ya Wakulima na Wafugaji  ambayo  imepelekea mauaji na baadhi ya Mifugo kufa na  kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga.

"Kazi ya kwanza Polisi walioua watafutwe, wapatikane na nipate taarifa; Haiwezekani Raia amekufa haijulikani aliyemuua ni  nani, hawa Wananchi hawatuelewi, ndio maana wanaoongea hapa mpaka unasikitika, nguvu inatumika ng'ombe amekatwa mkia wahalifu wanapatikana, anauawa mtu asipatikane kwa nini? Wakati mwingine matendo yetu ya kuchelewa yanasababisha wananchi wachukue Sheria mkononi; Uwe mkulima uwe mfugaji 
zingatia Sheria kama unaenda kienyeji  lazima utatuletea migogoro, serikali ipo haikututuma hapa kufanya masihara wala mizaha, tutashughulika na wavunja Sheria, Wahalifu bila kuzingatia vimo vyao, unene wao, wanang'ombe wangapi au mashamba kiasi gani" alisema Naibu Waziri Sagini.

Aidha, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi CP Awadhi Haji  amesema kuwa Jeshi la Polisi halipo tayari kuvumilia kuona matukio ya uvunjifu wa amani yanayosababishwa na migogoro ya Wakulima na Wafugaji yanatokea ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na amewahakikishia kuwa wanaovunja sheria za nchi watashughulikiwa ipasavyo.

Awali wakizungumza katika nyakati tofauti baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Nachingwea Kijiji cha Ngunichile pamoja na wakazi wa Wilaya ya Ruangwa Kijiji cha Matambaralale wamesema kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la mifugo katika Vijiji hivyo ikisababishwa na Wafugaji kuhama kutoka baadhi ya maeneo ya Wilaya za Lindi kutokana na uhaba wa malisho na maji na hivyo kuingiza mifugo yao katika Wilaya za Liwale, Nachingwea Lindi na Ruangwa kunywesha mifugo katika Mto Mbwemkuru ambao ndio tegemeo kubwa la upatikanaji wa maji.

Kwa upande wao baadhi ya Wafugaji  akiwemo Masanja Kabuta amesema kuwa changamoto kubwa inayowakabili Wafugaji hao ni baadhi ya Vijiji kutotenga maeneo mahsusi kwa ajili ya malisho na hivyo kuwafanya wenyewe kujiongoza namna gani usimsababishie mwenzio kero.

Hivi karibuni kumeripotiwa baadhi ya matukio ya kiuhalifu yakiwemo mauaji,ubakaji, uharibifu wa mazao na ushambuliaji wa mifugo kwa kukatwa mapanga katika Mkoa wa Lindi Wilaya za Ruangwa, Nachingwea,Liwale  na Lindi  ikisababishwa na migogoro ya Wakulima na Wafugaji

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi