Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mhe. Kairuki Amwapisha Kamishna Mpya wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
Oct 29, 2023
Mhe. Kairuki Amwapisha Kamishna Mpya wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki akimuapisha Kamishna mpya wa Hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Richard Kiiza.
Na John Mapepele

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki amemwapisha Kamishna mpya wa Hifadhi ya Ngorongoro, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Richard Kiiza kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika makao makuu ya  hifadhi hiyo jijini Arusha Oktoba 29, 2023.

 
Akizungumza mara baada ya kumvisha cheo na  kumwapisha, Waziri Kairuki amemshukuru Mhe. Rais  kwa kufanya  uteuzi huo ambapo amesema uteuzi huo  ni sehemu ya kuimarisha timu ya utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii kwa ajili ya kuhudumia watanzania kupitia sekta hiyo na kuhakikisha kuwa wizara inaendelea kuongeza jitihada za kuhifadhi, kutangaza utalii kwa njia mbalimbali za kisasa ili kuongeza idadi ya wageni wanaotembelea nchi ya Tanzania.


Aidha, amesema Serikali itaendelea kusimamia  kikamilifu  zoezi  la kuhama kwa hiari kwa wakazi  wa Ngorongoro kuelekea  katika maeneo wanayoyachagua huku ikizingatia haki zote za binadamu.


“Serikali inaendelea kuwahakikishia wadau mbalimbali, wananchi wa Ngorongoro na Jumuiya za Kimataifa kuwa zoezi hili ni la hiari, shirikishi na linazingatia misingi ya haki za kibinadamu na utawala bora na kila mwananchi aliejiandikisha kuhama kwa hiari Serikali itampa fidia na gharama zote za kumhamisha hadi alipochagua kwenda zinabebwa na Serikali kwa asilimia 100.” amefafanua Waziri Kairuki.

Ameongeza kuwa katika  awamu hii ya pili ya utekelezaji wa zoezi hili, Serikali imetoa fedha kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa zoezi la kuhamisha wananchi kwa hiari kwa awamu ya pili ikiwemo ujenzi wa Nyumba 5,000 katika Kijiji cha Msomera Wilayani Handeni, Saunyi Wilaya ya Kilindi na Kitwai Wilaya ya Simanjiro kwa ajili ya kuhakikisha wananchi walio tayari kuhama wanaandaliwa makazi bora na huduma za kijamii ili waishi maisha mazuri kama watanzania wengine tofauti na maeneo ya hifadhi.

Mhe. Kairuki  ameonya  baadhi ya watu wanaohujumu  zoezi hilo na kusisitiza  kuwa hatua za kisheria  zitachukuliwa dhidi yao ambapo  pia ameitaka mifugo yote ndani  kinyume cha sheria ya hifadhi kuondolewa.


Kwa upande  mwingine Waziri Kairuki amewasisitiza menejimenti na Watumishi wa NCAA kumpa ushirikiano Kamishna wa Uhifadhi mpya ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo ambayo amepangiwa na Serikali ya kuhakikisha kuwa malengo ya Shirika ya kuendeleza shughuli za uhifadhi, kutangaza utalii pamoja na maendeleo ya jamii yanatekelezwa ipasavyo na muda wote, huku akiwataka  kuongeza kasi ya utendaji kazi kwa kuwa wabunifu, waadilifu na kujituma zaidi katika kuhudumia watalii na wageni, mbalimbali wanaotembelea Hifadhi hiyo.


Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Raymond Steven Mwangala ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya  Ngorongoro amempongeza Mhe. Kairuki kwa kuteuliwa Waziri wa Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa serikali ya wilaya itaendelea kushirikiana  kikamilifu na Wizara  katika kuhifadhi  maliasili kwa faida ya vizazi vya sasa na baadaye.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi