Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amewataka Viongozi wapya aliowateua hivi karibuni kuwatumikia Watanzania na kutatua kero zao.
Mhe. Rais ameyasema hayo leo Septemba 01, 2023 Ikulu Ndogo ya Zanzibar wakati akiwaapisha Viongozi Wateule wakiwemo Mawaziri, Manaibu Waziri, Makatibu Wakuu, Manaibu Katibu Wakuu pamoja na Mabalozi.
“Mabadiliko haya ni ya kawaida ya kuimarisha maeneo yetu, ninachotarajia kwenu ni kujitoa kwenye kazi zenu; Sisi ni watumishi wa watu, katika utumishi wa watu, mahusiano ni jambo muhimu sana, lakini ukijipandisha kwamba umepata uteuzi, hutatumikia watu,” amesema Mhe. Rais.
Ameendelea kusema kuwa, upole si ujinga, bali ni maarifa ambayo mtu hutulia na kufikiria jambo mara mbili au tatu kabla hajatoa maamuzi au kauli; Hivyo amewaomba viongozi hao wakatulie na kuwatumikia wananchi.
“Ninachotaka ni mabadiliko tunayowaahidi wananchi, tunaahidi mambo mengi, twendeni tubadilike,” amesisitiza Mhe. Rais.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amesema, “kama kocha yoyote anavyofanya, imempendeza Mhe. Rais na amewaamini kubadilisha namba zenu za kucheza mpira, bila shaka anachohitaji Mhe. Rais ni tija zaidi katika utendaji”.
Aidha amewataka viongozi hao kuzingatia falsafa ya Mhe. Rais ya 4R, ambapo ametilia mkazo katika kusimamia mabadiliko (Reforms) kwa viongozi hao katika maeneo yao ya kazi waliyopangiwa.
“Ni muhimu sana muwe na masikio juu ya kero za wananchi wetu Bara na Visiwani na kuzifanyia kazi, yako maeneo ambayo kelele ni kubwa kila unapokwenda,” amesema Mhe. Dkt. Mpango.
Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewaahidi viongozi hao ushirikiano kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Kwa wale ambao mpo nafasi za Muungano niwahakikishie ushirikiano kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili tuweze kuudumisha na kuuendeleza muungano wetu, kwa wale ambao hawapo nafasi za muungano, nao niwahakikishie ushirikiano ambao ni utamaduni wetu, hata kwa maeneo ambayo sio ya muungano tuna ushirikiano mzuri,” amesema Mhe. Dkt. Mwinyi.