Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Azungumza na Balozi Polepole
May 05, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi anayekwenda kuiwakilisha Tanzania nchini Malawi, Mhe. Balozi Humphrey  Polepole. Mazungumzo hayo yamefanyika Ofisini kwa Makamu wa Rais mkoani Dodoma.

Makamu wa Rais amempongeza Balozi huyo kwa kuteuliwa na imani aliyopewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuliwakilisha taifa nchini Malawi. Makamu wa Rais amemsihi Balozi Polepole kwenda kufanya kazi kwa weledi na uzalendo kwa maslahi ya Taifa.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika kutekeleza Diplomasia ya uchumi hivyo amemtaka Balozi Polepole kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi utakaokuwa na manufaa kwa Tanzania.

Amesema nchi za Afrika zina uwezo wa kufanya uwekezaji baina ya mataifa yao na kupata manufaa makubwa hivyo amemsihi Balozi Polepole kuvutia wawekezaji wa Malawi hapa nchini pamoja nakutafuta fursa za uwekezaji nchini Malawi.

Aidha, amemuasa kutambua vipaumbele vya Taifa ikiwa ni pamoja na kufahamu takwimu za msingi zilizopo katika Dira ya Taifa na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano pamoja na vipaumbele vilivyopo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020, zitakazochagiza katika kutafuta wawekezaji.

Halikadhalika amemuagiza Balozi Polepole kuhakikisha anashiriki katika mikutano mbalimbali itakayowezesha kujifunza, kueleza mazuri yaTanzania pamoja kuvutia wawekezaji. Amesema ni muhimu kuendelea kuitangaza lugha ya Kiswahili katika nchi hiyo ikiwemo kutafuta fursa ya kufundishwa kwa lugha hiyo nchini Malawi. 

Aidha, amemuasa kuwaunganisha watanzania wanaoishi nchini Malawi ili kuwa na mawazo ya pamoja namna wanavyoweza kuwekeza hapa nchini na kurudisha ujuzi na maarifa walioyonayo nyumbani Tanzania.

Makamu wa Rais amemsihi Balozi Polepole kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha zinazopelekwa katika kuendesha ubalozi huo ili kuongeza tija ya uwakilishi nchini humo.

Kwa upande wake Balozi Humphrey Polepole amemshukuru Makamu wa Rais kwa miongozo aliompa na kuahidi kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi ya taifa la Tanzania. 
Amesema tayari ameanza kuchukua hatua mbalimbali kwa lengo la kutatua changamoto zilizopo zinazoweza kutatuliwa kupitia Mamlaka za Tanzania kama vile Bandari na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi