Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amemuagiza Waziri wa Maji kuchukua hatua kwa bodi za maji zitakazobainika kuchelewesha uunganishaji maji kwa wananchi pamoja na ubambikiziaji wa ankara za maji.
Makamu wa Rais amesema hayo mara baada ya kuzindua Mradi wa Maji wa Kikafu – Bomang’ombe uliopo katika Kijiji cha Kwasadala Wilaya ya Hai akiwa ziarani mkoani Kilimanjaro. Mradi huo umegharimu shilingi bilioni 2.8 na unahudumia wananchi zaidi ya 63,049.
Makamu wa Rais ameagiza Wizara kusimamia bodi za maji ili kuhakikisha zinakuwepo gharama halisi za uunganishaji wa huduma ya maji kwa wananchi pamoja na kuzingatia muda wa uunganishaji huduma hizo.
Pia ametoa wito kwa wananchi wa Wilaya ya Hai na Tanzania kwa ujumla kulinda vyanzo vya maji ili huduma za upatikanaji wa maji ziwe endelevu. Makamu wa Rais ameelekeza fedha kiasi cha shilingi milioni 500 zilizobaki katika utekelezaji wa mradi wa maji Kikafu – Bomang’ombe zikatumike katika kupeleka huduma za maji kijiji jirani cha Matoho.
Akizungumzia suala la mgogoro wa eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Makamu wa Rais amewasihi wananchi kuwa wamoja katika masuala ya maendeleo na kuachana na ubinafsi. Amesema ni muhimu kutanguliza maslahi ya nchi mbele wakati wote huku akisisitiza kwamba kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro ni moja ya kiwanja kinachoingiza fedha nyingi za kigeni. Aidha ameuagiza uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kufikiria kuongeza siku za notisi kutoka 21 kufikia siku 90 kwa wananchi waliolipwa fidia kuhama katika eneo hilo.
Makamu wa Rais ameagiza kupelekwa kwa fedha shilingi bilioni 11.2 zilizotengwa kwa ajili ya soko la Kwasadala wilayani Hai. Pia ameagiza kufanyika kwa tathimini ya ujenzi wa barabara ya Arusha - Horiri na upanuzi wa barabara ya Moshi - Arusha ili kazi ya upanuzi iwepo kwenye mpango kazi wa utekelezaji kuanzia bajeti ijayo. Halikadhalika ameagiza kufanyika kwa tathimini ya shule zilizochakaa mkoani Kilimanjaro ili shule hizo zikarabatiwe na kuwa bora na nzuri.
Makamu wa Rais amewataka wananchi wa Kilimanjaro kuwajibika kutunza vyanzo vya maji, misitu ya asili pamoja na kupanda miti maeneo yaliathirika na uharibifu ili kuweza kuokoa taifa na athari kubwa za mabadiliko ya tabia nchi.
Vilevile, Makamu wa Rais ametoa wito kwa wananchi wenye uwezo kuanza kuhama kutoka katika nishati chafu kwenda katika nishati safi ya kupikia. Amezitaka taasisi ambazo zinazolisha watu 100 na zaidi kwa siku kuacha kutumia kuni katika kupika. Ametoa wito kwa taasisi mbalimbali kushiriki katika programu ya kusambaza majiko ya gesi.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kilimanjaro kutumia vema mwaka huu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kuchagua viongozi bora. Amewasihi viongozi wa dini kuendelea kuhamasisha amani pamoja na kuwasihi watu wanaotumia njia ya demokraisa kutafuta haki, watafute haki hizo kwa njia ya amani na lugha ya staha. Amesema ni vema wakati Serikali ya Awamu ya Sita inajenga demokrasia ya kweli ili Watanzania wawe na uhuru wa kutoa mawazo yao wanapaswa kutambua wajibu wao wa kuijenga nchi na kutunza amani.
Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Kilimanjaro kuachana na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi na mirungi kwani vinahatarisha taifa na rasilimali watu.
Kwa Upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wizara imeweza kufanikisha kufikisha huduma ya maji vijijini kutoka asilimia 54 hadi asilimia 79, pamoja na kutoka asilimia 60 hadi 88 kwa maeneo ya mjini.
Aweso amesema miradi ya maji zaidi ya 1,500 inaendelea kujengwa nchi nzima na Wizara imejipanga kuhakikishja miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili Watanzania waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
Makamu wa Rais anaendelea na ziara katika mkoa wa Kilimanjaro.