Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewaongoza waombolezaji katika kutoa heshima za mwisho wakati wa kuaga mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Ali Hassan Mwinyi katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam.
Akitoa salamu za pole kwa waombolezaji, Makamu wa Rais amesema Hayati Ali Hassan Mwinyi atakumbukwa kwa kuwa kisima cha hekima, chemichemi ya elimu na shule ya uzalendo uadilifu na uongozi. Amesema Hayati Mwinyi alijitoa kwa dhati kulitumikia Taifa kwa moyo wake wote na kutoa mchango mkubwa kwa nafasi zote alizoshika katika utumishi wa umma.
Makamu wa Rais ameongeza kwamba Hayati Ali Hassan Mwinyi alikuwa kielelezo cha kutetea na kudumisha umoja wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, alikuwa na karama kubwa ya uongozi na alizingatia kwa dhati masharti ya uongozi ikiwemo uwajibikaji pamoja na kutoa mchango mkubwa katika kukuza matumizi ya lugha ya kiswahili na kuifanya kutambulika na kutumika kimataifa.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema Hayati Ali Hassan Mwinyi aliasisi mageuzi ya kiuchumi na kisiasa hapa nchini, alijijengea sifa kubwa katika kuhamasisha kilimo bora pamoja na kuwa na bidii katika kumwabudu Mwenyezi Mungu.
Tukio la kuagwa kwa Mwili wa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Ali Hassan Mwinyi katika Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es salaam limehudhuriwa na Waziri Mkuu wa Ethiopia Mhe. Abiy Ahmed Ali, viongozi mbalimbali wa kitaifa, Mabalozi wa Mataifa mbalimbali, Viongozi wa Ulinzi na Usalama, Viongozi wa Dini mbalimbali pamoja na Wananchi.