Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Akutana na Wawakilishi wa Jukwaa la Uchumi Duniani
May 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema katika karne ya 21, Bara la Afrika linapaswa kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo pamoja na kuunganisha mawazo kwa pamoja ili kutatua changamoto zinazokabili bara hilo.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 2 Mei 2022 alipokutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi kutoka Sekretarieti ya Jukwaa la Uchumi Duniani wakiongozwa na Mkuu wa Ajenda za Afrika, bwana Chido Munyati, mazungumzo yaliyofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania Jijini Dodoma.

Amesema kwa sasa bara la Afrika ikiwemo Tanzania linahitaji zaidi teknolojia ili kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo pamoja na kuendana na uchumi wa kidijitali. Ameongeza kwamba umoja baina ya nchi za Afrika utachochea ukuaji wa biashara katika eneo huru la Afrika na kuinua uchumi baina ya mataifa. 

Aidha, ameongeza kwamba uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu kama vile Reli na Barabara baina ya mataifa utaongeza kasi ya ufanyaji biashara na ukuzaji wa uchumi ndani ya bara la Afrika. Makamu wa Rais amesema Tanzania inaendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Pwani ya bahari yaHindi kupitia katikati ya Tanzania hadi Magharibi mwa Tanzania na kanda ya ziwa itakayosaidia nchi za Afrika Mashariki katika usafiri na biashara.

Wawakilishi hao wamemkaribisha Makamu wa Rais katika mkutano mkuu wa Jukwaa la Uchumi Duniani unaotarajiwa kufanyika Davos nchini Uswisi tarehe 22 – 26 Mei 2022 ambapo wamesema mkutano huo utatoa fursa kwa Tanzania kueleza fursa zinazopatikana nchini ili kuvutia wawekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za Kilimo, Nishati ,utalii pamoja na Uchumi wa buluu. 

Aidha mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi katika kuyafikia maendeleo kwa mataifa ya Afrika.

Mkutano Mkuu wa Jukwaa la Uchumi Duniani unatarajiwa kuwakutanisha Wakuu wa nchi na Serikali kutoka mataifa mbalimbali, wawakilkishi wa mashirika ya kimataifa , Wakuu wa taasisi na makampuni mbalimbali duniani, pamoja na wafanyabiashara.

Mazungumzo hayo yamehudhuriwa na viongozi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi