Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Ahutubia Mkutano wa Maralia Rwanda
Jun 23, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inaendelea kuongeza jitihada mbalimbali katika kukabiliana na ugonjwa wa Malaria pamoja na Magonjwa ya Kitropiki yaliosahaulika (NTDs) ambayo yamekuwa changamoto kubwa ya afya ya umma nchini Tanzania ambapo zaidi ya watu milioni 29 wanahitaji matibabu ya angalau moja ya ugonjwa wa Kitorpiki uliosahaulika.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa Mkutano uliolenga kuunganisha nguvu za pamoja katika kukabiliana na ugonjwa wa Malaria pamoja na Magonjwa ya Kitropiki Yasiyopewa Kipaumbele uliofanyika Kigali nchini Rwanda ikiwa ni miongoni mwa mikutano ya Wakuu wa Serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya za Madola unaoendelea nchini Rwanda. 

Makamu wa Rais ametoa wito wa kuimarisha ushirikiano wa wadau mbalimbali kufanya uwekezaji katika upatikanaji wa kinga, upimaji wa magonjwa, matibabu, ufuatiliaji wa magonjwa pamoja na kuunganisha uvumbuzi na tafiti ili kuharakisha kufikia malengo na ahadi za mwaka 2018 ambazo zililenga kuondoa malaria katika nchi wanachama wa Jumuiya za Madola ifikapo 2023.

Pia, amesema Tanzania kwa sasa inatekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Programu ya Kudhibiti Magonjwa ya Kitropiki Yasiopewa Kipaumbele (2021 – 2026) unaolenga kuendeleza mafanikio yaliyopatikana katika Kudhibiti na Kutokomeza magonjwa hayo na kuongeza ufuatiliaji wa magonjwa.

Makamu wa Rais amesema tayari mafanikio mbalimbali yamepatikana nchini Tanzania katika udhibiti wa ugonjwa wa Malaria ikiwemo kufikia chini ya asilimia moja kuenea kwa ugonjwa huo Zanzibar pamoja na mikoa mitano ya Tanzania bara ambapo lengo katika maeneo hayo ni kuondoa kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2025.

Katika Mkutano huo umeshirikisha viongozi mbalimbali wa Serikali na mashirika ya kimataifa akiwemo Prince Charles wa Wales, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Mokgweetsi Masisi wa Botswana, mwenyekiti mwenza wa Bill and Melinda Gates Foundation Bi. Melinda Gates pamoja napamoja na wadau mbalimbali.

Makamu wa Rais yupo nchini Rwanda kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Serikali wa Nchi Wanachama za Jumuiya yaMadola.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi