Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Makamu wa Rais Afungua Warsha ya Utunzaji Bahari
Jul 19, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 19 Julai, 2022 amefungua warsha ya Umoja wa Mataifa kuhusu tathmini, usimamizi na utunzaji wamazingira ya Bahari, warsha inayofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam kuanzia leo  tarehe 19 hadi 27 Julai 2022.

Akizungumza na Viongozi na washiriki wa Warsha hiyo, Makamu wa Rais amesema umoja baina ya mataifa pamoja  na kujitolea ni mambo muhimu yatakayopelekea matumizi endelevu ya rasilimali za bahari pamoja na kuepusha kupotea kwa rasilimali hizo. 

Amesema ni lazima kuzuia na kupunguza uchafuzi wa bahari kwa kila namna kuanzia vyanzo vya ardhini hadi baharini. Ameongeza kwamba unahitajika muongozo endelevu wa biashara ili uchumi wa bahari uendane na mazingira ya baharini.

Pia Makamu wa Rais amesema kwa sasa katika kulinda bahari vinahitajika vitendo zaidi vitakavyokwenda sambamba na sayansi, uvumbuzi na teknolojia pamoja na ushirikishwaji wa wadau wote unaojumuisha vijana na wanawake katika mijadala ambao ni sehemu ya suluhu.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesisitiza kwamba Tanzania imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kulinda mazingira ikiwemo mazingira ya bahari kama vile kupiga marufuku utumiaji wa mifuko ya plastiki inayotumika mara moja, kutenga asilimia 6.5 eneo la Bahari ya Hindi kuwa eneo tengefu la bahari, kudhibiti kwa asilimia 99 uvuvi haramu pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi wa bahari kuu.

Amesema umefika wakati wa kutafuta njia sahihi za kudhibiti na kusimamia shughuli zinazofanyika baharini, pamoja na  namna bora ya kuweka uwiano wa kiuchumi, kijamii na kimazingira wakati wakutumia rasilimali za bahari.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Selemani Jafo amesema warsha hiyo imelenga kutambua mahitaji ya Serikali katika kufanya tathmini ya mazingira ya bahari ikiwemo shughuli za kiuchumi, kuongeza uelewa wa matumizi sahihi  ya bahari pamoja na kuvutia jamii ya wanasayansi katika kuandika tathmini kwa lengo la kuimarisha sera za kisayansi kwa utunzaji bora wa bahari na rasilimali zake na kuhakikisha uchumi wa buluu ni endelevu na wenye manufaa.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Aboud Jumbe amesema kinachohitajika ni kuendelea kufanya kazi pamoja kitaifa, kikanda na kimataifa ikiwa pamoja na kuwashirikisha wadau, watumiaji wa bahari pamoja na jamii inayoishi pembezoni mwa bahari kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi kwa kutumia uchumi wa buluu. 
Ameongeza kwamba Wataalam wanapaswa kuzingatia mahitaji ya watumiaji wa bahari ambao wanaishi pembezoni kwa kuwa wamebeba wajibu wa ulinzi wa rasilimali za baharini.

Awali mwakilishi wa Umoja wa Mataifa, kitengo cha mambo ya Bahari na Sheria za Kimataifa za Bahari, Bi. Alice Hicuburundi amesema kwamba uelewa ni jambo muhimu zaidi katika kulinda, kuhifadhi na matumizi endelevu ya bahari. 

Amesema matumizi ya sayansi na teknolojia yakiungana na uelewa ndio yanapaswa kuwa msingi wa ulinzi na utawala wa bahari kwa maendeleo endelevu hasa katika kufikia lengo la 14 la Umoja wa Mataifa.  

Madhumuni ya warsha hiyo ni kuwajengea uwezo washiriki  juu ya usimamizi wa bahari ikiwemo kuonesha hali na mwelekeo wa bahari, vihatarishi vikuu vinavyoikabili bahari na mazingira yake, matokeo ya vihatarishi hivyo, na hatua mbalimbali za kupunguza athari hizo. 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi